Tuesday , 27th Jan , 2015

Wananchi wa kijiji cha katulukila kata ya Mkula Wilayani Kilombero, wameilalamikia serikali kwa kutochukua hatua madhubuti na za haraka za kuwadhibiti wanyama aina ya tembo kuingia ndani ya kijiji hicho na kuharibu mazao ya wanakijiji hao.

Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Elias Masala (kulia), akijibu maswali mbele ya Kinana jinsi alivyopanga mikakati ya kuwaletea mandeleo wananchi wa wilaya hiyo.

Akizungumza kijijini hapo mwenyekiti wa kijiji cha Katulukila bwana Jofrey Mtagawa amesema kuwa, tataizo hilo limedumu kwa muda wa zaidi ya mwaka mmoja sasa licha ya askari wa wanyama pori kufika na kuwatishia kwa milio ya bunduki lakini wamekuwa jeuri kukimbia kutokana na kuizoea milio hiyo ya kutishwa pekee.

kwa upande wao wanakijiji wa kijiji hicho wamesema tembo hao ni hatari kwa usalama wao kwani wamekuwa na hofu ya kujeruhiwa na hata kuuawa na wanyama hao kwani kwa kipindi hiki wamekuwa wakiingia mpaka kwenye makazi ya watu na kuzidi kufanya uharibifu wa vitu vingi hususani mashamba ambayo wanayategemea kwa chakula pamoja na kuwahudumia watoto wao gharama za shule

Wananchi hao wamelalamika kuwa mkuu wa Wilaya ya Kilombero Bwana Hasani Eliasi Masala na licha ya kufika kijijini hapo na kusikiliza kilio cha wanakijiji hao juu ya Wanyama hao wanavyo haribu mazao yao mkuu huyo ametoa onyo la kutowaua tembo hao bali wakiwaona wawafanyie tendo la wanawaamkia.

Mbali na tatizo hilo kijiji hicho pia kinakabiliwa na tatizo la umeme na kwa muda mrefu sasa wamekuwa wakiahidiwa na serikali kuwa umeme utafika ndani ya kijiji hicho lakini utekelezaji wake umekuwa mgumu licha ya kukamilisha taratibu zote kutoka shirika la umeme Tanzania TANESCO.

Aidha wanakijiji hao wameongeza kuwa wamewaomba viongozi wa serikali kutembelea wananchi wao na kuacha kukaa ofisini pekee, kwani kwa kufanya hivyo hawatajua matatizo yanayowasumbua na itakuwa kazi kutolea ufafanuzi na utatuzi stahiki pamoja na kuwataka kutekeleza ahadi zao wanazoahidi na kero zinazotolewa na wananchi kutekelezwa kwa wakati ili wazidi kujenga imani na viongozi wao wanaowatawala.