Wizara ya Maji na Umwagiliaji nchini Tanzania kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mkoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI, Sekretarieti za Mikoa na Halmashauri za Wilaya mbalimbali zimefanikiwa kuwapatia maji wananchi waishio vijijini wapatao 752,000 wa ziada katika kipindi cha miezi mitatu tangu tarehe 1 Julai mwaka huu.
Ongezeko hilo ni sawa na asilimia 2 ya wakazi wote wanaoishi vijijini kupata huduma ya maji safi kwa kipindi hicho cha miezi mitatu. Baadhi ya miradi iliyokamilika ni ya vijiji vya Mtandi, Rondo, na Kinengene vilivyopo Mkoani Lindi; Vijiji vya Engagile, Gedamar, Mtuka vilivyopo Mkoani Manyara; na Vijiji vya Iwalanje, na Maninga vilivyopo Mkoani Mbeya.
Hatua hiyo inakuja zikiwa ni siku chache kupita baada ya Tanzania kuwa mwenyeji wa Maadhimisho ya Sita ya Wiki ya Maji ya Afrika wa Mkutano Mkuu wa Kumi wa Baraza la Mawaziri wa Maji wa Afrika Utakayofanyika jijini Dar Es Salaam na waziri wa Maji na Umwagiliaji nchini Mhandisi Gerson Lwenge kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa Maji Afrika (AMCOW)



