Thursday , 4th Dec , 2014

Wanafunzi wa baadhi ya shule mbalimbali za sekondari jijini Tanga wamesifu jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Kikwete za kuleta mapinduzi ya elimu kupitia ujenzi wa maabara.

Maabara

Wanafunzi wa baadhi ya shule mbalimbali za sekondari jijini Tanga wamesifu jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Kikwete za kuleta mapinduzi ya elimu kupitia ujenzi wa maabara lakini wamehimiza kuwa zoezi hilo lienda sanjari na kuongeza idadi ya walimu wa masomo ya sayansi ili waweze kupata tija katika mchepuo huo.

Wakizungumza na EATV katika shule ya sekondari ya Nguvumali katika hafla fupi ya uzinduzi wa maabara ya kisasa iliyojengwa kwa ufadhili  wa serikali ya Korea Kusini, baadhi ya wanafunzi hao wamesema shule nyingi zimejenga maabara chini ya agizo la mheshimiwa Rais lakini zitakapomalizika viwepo vitendea kazi pamoja na idadi kubwa ya walimu ili idadi kubwa ya wanafunzi waweze kujikita na mchepuo wa sayansi.

Kwa upande wake afisa elimu sekondari jijini Tanga bwana Bashiri Shelimu amewataka wanafunzi kutumia vifaa vya maabara kuwa kichocheo cha kukuza masomo ya sayansi katika shule ya sekondari Nguvumali na akaishukuru serikali ya Korea Kusini kwa kujenga maabara moja pamoja na vifaa vyake kisha kusaidia sehemu ya ujenzi wa maabara zinazojengwa chini ya agizo la mheshimiwa Rais Kikwete ili kuwapunguzia changamoto wanafunzi wa shule za sekondari.

Kufuatia hatua hiyo mwakilishi wa wakala wa ushirikiano wa kimataifa nchini bwana Kim Seungibeon amesema lengo la maabara hiyo iliyojengwa kwa gharama ya shilingi milioni 29.5 ambapo kati ya hizo halmahauri ya jiji la Tanga imechangia shilingi mil 1.6 ni kuwapa uwezo walimu na wanafunzi waweze kuyafanyia kazi na kuyaelewa kwa kina masomo wanayojifunza darasani ili maabara hiyo ya kisasa itumike kuwa chombo cha kutengeneza na sio kutumia maarifa

Tags: