Tuesday , 30th Oct , 2018

Kampuni ya IPP imetangaza kuanza ujenzi wa kiwanda cha kwanza cha kutengeneza simu janja maarufu kama smartphone, simu ambazo zitalenga kurahisisha mawasiliano ya mtanzania mwenye kipato cha chini na wanafunzi watapatiwa mikopo ya vifaa vya kielektroniki.

Laptop pichani.

Vifaa hivyo vya kielektroniki vitakuwa ni pamoja na kompyuta mpakato, 'headphones' na simu zitakazokuwa na uwezo wa kukaa na chaji kwa muda wa wiki moja na kwa wasiokuwa na umeme wataweza kuchaji kwa nguvu ya jua.

Akizungumza na wanahabari, Afisa Mtendaji Mkuu wa IPP TouchMate, Victoria Tesha amesema kuwa kampuni hiyo imelenga kutoa mikopo ya kompyuta mpakato kwa wanafunzi wa vyuo vikuu ambao watapewa fursa ya kulipa taratibu.

"Tunategemea siku tisini kuanzia sasa bidhaa zetu ziwe tayari sokoni na zitauzwa kuanzia shilingi elfu themanini kwa simu za mkononi 'smartphone' hadi laki mbili bei ya juu, na kwa upande wa laptop na ipad tutakopesha chini ya shilingi laki tano kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na watalipa kwa muda mrefu", amesema Tesha.

Aidha Mwenyekiti Mtendaji wa makampuni ya IPP Dkt. Reginald Mengi amesema kiwanda hicho kitakuwa na mchango mkubwa kwenye uchumi na sehemu kubwa ya watakaoajiriwa ni watu wenye ulemavu.