Thursday , 15th Jan , 2015

Jumla ya wanafunzi 84 wa kitivo maalum cha stashahada ya Ualimu katika chuo kikuu cha Dodoma (UDOM) wanashikiliwa na jeshi la Polisi Mkoani hapa kwa tuhuma za kuhamasisha uvunjifu wa amani Chuoni na kufanya maandamano haramu

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, SACP David Misime

Wanafunzi hao wamekamatwa leo wakiwa njiani kutoka Chuoni kuelekea katika Ofisi mbalimbali za viongozi wa Serikali zilizopo Dodoma Mjini majira ya saa kumi na moja alfajiri.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi David Misime – (SACP) amethibitisha kukamatwa kwa wanafunzi hao na kusema kuwa chanzo cha wanafunzi hao kufanya uhalifu huo ni kikao walichofanya wanafunzi hao Desemba 13 wakidai kuongezewa posho ya chakula na kwamba hata kiasi ambacho wanapewa kimechelewa kutolewa.

Kwa mujibu wa Misime uongozi wa Chuo uliwaeleza kuwa wenye mamlaka ya kuzungumzia suala la kuongezewa posho ni Bodi ya Mikopo na siyo chuo ambapo walitakiwa kufuata taratibu za kuwasilisha madai yao.

Misime amesema kuwa wanafunzi hao walielezwa kuwa hundi kwa ajili ya fedha za posho zao zimeshasainiwa na kuwasilishwa Benki ili waweze kuanza kupewa posho zao.

“Hata hivyo wanafunzi hao hawakuridhika na usiku wakaanza kuhamasishana kufanya maandamano jambo ambalo ni kosa kisheria. Wanafunzi hao wamehojiwa kulingana na ushahidi ambao umekusanywa na watafikishwa mahakamani kwa kosa la Kufanya Maandamano yasiyo na kibali,” alisema Misime.

Ameongeza kuwa, “Viongozi waliohamasisha uvunjifu huo wa sheria baadhi wamekamatwa na baadhi wanaendelea kutafutwa ili nao waweze kuchukuliwa hatua stahiki.

Ushahidi uliokusanywa unaonyesha jinsi viongozi hao walivyoshiriki kuhamasisha kupitia vikao rasmi na visivyo rasmi, katika vikundi, kupita katika mabweni na kutuma sms.”

Mbali na hilo Misime ametoa wito kwa Wanafunzi hao kutumia taratibu zilizowekwa na Serikali na Chuo kuwasilisha malalamiko yao ngazi kwa ngazi na siyo kufanya vitendo vya kuvunja sheria ambavyo vitawasababishia kukamatwa.

Endapo watafanya hivyo wasije kulaumu mtu kwani hatua zitachukuliwa kulingana na Sheria inavyoelekeza ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani,” alisema Kamanda Misime.