Tuesday , 1st Jul , 2014

Watu wanaosadikiwa kuwa ni wa kabila la wamasai wameziba lango kuu la kuingilia eneo la kitalii katika kreta la Ngorongoro ambalo lipo ndani ya mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro mkoani wa Arusha wakipinga kuendelea kwa ujenzi wa hoteli za kitalii.

Waziri wa maliasili na utalii Lazaro Nyalandu.

Wakati tukio hilo likitokea hii leo, Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Lazaro Nyalandu alikuwa ndani ya eneo la kreta ya Ngorongoro kwa ajili ya kushuhudia uzinduzi wa bodi mpya ya mamlaka hiyo.

Kitendo hicho kinadaiwa kufaywa ili kumshinikiza Waziri Nyalandu atoke na kusikiliza madai yao ya kupinga ujenzi wa hoteli za kitalii kwa madai ya kutaka kupatiwa uwakilishi ndani ya bodi hiyo lakini pia kwa serikali kutenga ardhi maalumu kwa ajili ya malisho ya mifugo yao.

Aidha, akijibu hoja za wananchi hao, Mhe. Nyalandu amesema hakutakuwa na ujenzi wowote wa hoteli pasipo kuangalia athari za kimazingira na kijamii kwa wakazi wa eneo hilo, na kufafanua kuwa serikali inafahamu juu ya madhara yanayoweza kutokea iwapo utaratibu huo hautofuatwa.