Thursday , 1st Oct , 2015

Wafanyabiashara ndogondogo maarufu machinga jijini Mwanza, wametakiwa kutotumika na wanasiasa hususani kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu bali wawe chanzo cha kuilinda amani.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza,Charles Mkumbo.

Kamanda wa polisi mkoani Mwanza, Charles Mkumbo, akizungumza na machinga hao pamoja na wajasiriamali , amesema kila mmoja ana haki ya kuilinda amani ya nchi na wala siyo vinginevyo.

Amesema vitendo vya uvunjifu wa amani vitakwamisha usalama wa watu pamoja na shughuli mbalimbali za maendeleo, jambo ambalo litaathiri jamii ikiwamo ya wafanyabiashara, watoto, wazee, walemavu jambo ambalo litanatokana na ushabiki wa kisiasa.

Aidha, kamanda Mkumbo ametoa wito kwa wafanyabiashara kujenga tabia ya kutoa taarifa kwa vyombo vya dola pindi pale wanapoona viashiria vya uvunjifu wa amani kwani itasaidia kupunguza vitendo viovu vinavyofanywa na baadhi ya wanajamii.

Naye mwenyekiti wa Chama cha Machinga hao, Saidi Tembo, amesema suala la vijana kutumika kisiasa na kusababisha uvunjifu wa amani bila ya kujali manufaa yao ya baadaye lazima yaangaliwe kwa ajili ya mustakabali wa taifa na wananchi wake.