Chama cha waalimu mkoa wa kilimanjaro (CWT) kinaidai serikali zaidi ya shilingi milioni 985 zilizokatwa kwenye mishahara ya waalimu kwa miezi miwili hali iliyochangia vyama saba vya mkoa wa kilimanjaro kushindwa kutoa mikopo kwa waalimu na kuwafanya watumishi hao kwenda kukopa kwenye taasisi nyingine na kushindwa kurejesha kwa wakati.
Hayo yamebainishwa na mameneja wa vyama hivyo na kusema kuwa imekuwa kero kubwa kutokana na vyama hivyo kushindwa kutoa mikopo na hivyo kusababisha baadhi ya walimu kwenda kwenye taasisi nyingine za kifedha kutafuta mikopo kwa ajili ya mahitaji yao.
Wamesema zaidi ya walimu 12,000 ambao ni wananchama wa vyama vya akiba na mikopo wamekatwa mishahara yao na fedha hizo tangu mwezi Julai hazijawasilishwa kwenye SACCOS hizo hali ambayo inaleta usumbufu mkubwa kwa Walimu.
Kwa upande wake katibu wa chama cha walimu CWT mkoa wa kilimanjaro Bw. Nathanael Mwandete ameiomba serikali kuwasilisha fedha hizo kwa wakati kwa kuwa hali hiyo inaweza kuhatarisha shughuli za ufundishaji kutokana na walimu hao kufuatilia madai hayo ambayo ni haki yao.
Naye mwenyekiti wa chama cha waalimu (CWT) mkoa wa kilimanjaro Bw.Omari Mchomvu amesema kama serikali haitalipa madai hayo kwa wakati chama hicho kitahamasisha walimu kuandamana.