Friday , 24th Aug , 2018

Imeelezwa kuwa katika suala zima la mahusiano halina uchawi wowote zaidi ya kujiamini na kujikubali wala halitazami muonekano wa mtu husika kama ambavyo jamii inafanya hali inayopelekea baadhi ya watu kukataa kuwa kwenye mahusiano na watu wenye ulemavu.

Elia Msoke (kulia) akiwa na mkewe Evodia Msoke.

Elia Msoke ni mlemavu wa macho ambaye ana elimu ya shahada ya sheria na mmiliki wa taasisi ya kusaidia na kuwaendeleza walemavu ili kupingana na vitendo vya uonevu dhidi yao ambapo amesema kuwa kinachopelekea walemavu kujitenga muda mwingine ni kukosa kujiamini na kutanguliza ulemavu wao kama kigezo cha kutaka huruma kwa jamii.

Akizungumza kupitia DADAZ ya EATV, Msoke amesema, walemavu wa macho  wana mapenzi ya dhati kuliko watu wanaoona kwakuwa wao huongozwa na hisia zaidi kuliko tamaa za macho na ndicho ambacho wametofautishwa nacho huku akitoa rai kwa wenzake kutokuwa waoga wajifunze kuthubutu kwani kwa kufanya hivyo ni kujitenga wao.

Mapenzi ni tasnia kubwa sana kinachotesa watu kwa sasa ni tamaa zinazokuwa ndani ya vijana na kutokujiamini kwao”, amesema Msoke.

Kwa upande wake Evodia Msoke ambaye ni mke wa Elia amesema, haikuwa rahisi kukubali mara moja kwani alihofia endapo wazazi wake watakubaliana nae kutokana na hali ya Elia lakini familia ilikuabliana naye na ndugu wachache ndio waliokuwa na kikwazo.

Kwa mujibu wa shirika la HakiElimu kupitia mpango  kazi wake wa 2017-2021 Elimu jumuishi ni mpango wa kitaifa ambao una lenga kuondoa ubaguzi na kuwawezesha wanafunzi wote bila kujali hali zao kimaumbile wala kiafya na kupitia mpango huo utaboresha usawa katika jamii ili kuondokana na dhana potofu ya unyanyapaa kwa walemavu.