Thursday , 8th Jan , 2015

Wakulima wa wilaya ya Gairo Mkoani Morogoro nchini Tanzania wametishia kulivunja Ghala la wakala wa mazao nchini NFRA kutokana na kutolipwa pesa zao kwa wakati hali inayowapelekea kushindwa kuandaa mashamba kwa msimu mwingine.

Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Khadija Karamagi.

Wakizungumza mbele ya katibu tawala wa Wilaya hiyo Severine Garika jana wakulima hao wamesema kuwa Serikali iliwaahidi kuwa wakala huyo atanunua mazao yao na kusema mpaka sasa ni zaidi ya miezi minne hawajalipwa pesa zao na kuwafanya waanze kuishi maisha magumu.

Wakulima hao wamesema serikali imekuwa ikiwazungusha na kuingiza siasa katika suala hilo na kusema kuwa wamefikia hatua ya kushindwa kuwapeleka shule watoto wao kutokana na kutolipwa fedha hizo kutoka kwa wakala huyo.

Kufuatia tamko hilo la wakulima sambamba na maandamano mpaka kwa mkuu wa wilaya hiyo katibu tawala wa wilaya hiyo Bw. Severin Garika ambaye amewataka wakulima hao kuwa na subira kwa kuwa serikali imesema ipo katika hatua za mwisho za kulipa madeni hayo.