Wednesday , 2nd Apr , 2014

Wakazi wa jiji la Dar es Salaam nchini Tanzania, wametakiwa kuchukua hatua za tahadhari kufuatia tishio la kuwepo kwa mafuriko yatakayosababishwa na mvua kubwa zinazoendela kunyesha katika maeneo yote ya mkoa wa Dar es Salaam.

Tahadhari hiyo imetolewa na mkuu wa mkoa mh. Said Meck Sadiki, kufuatia utabiri wa mamlaka ya hali ya hewa kuonyesha kuwa kutakuwa na mvua kubwa zinazoweza kuleta madhara kwa wakazi waishio mabondeni na maeneo mengine hatarishi.

Mkuu wa mkoa Sadiki amesema sheria ya mipango miji hairuhusu ukaaji na uendelezaji wa maeneo hatarishi na hivyo ameziagiza mamlaka za serikali za mitaa kupitia kamati za maafa kuratibu na kusimamia suala hili kuhakikisha kuwa wakazi wanaoishi maeneo ya bondeni na hatarishi wanahama haraka iwezekanavyo.