Sunday , 7th Feb , 2016

Baadhi ya wajumbe wa ZEC wamesema Mwenyekiti wao Jecha Salim Jecha hakuwahusisha kwenye baadhi ya maamuzi aliyofanya.

Baadhi ya wajumbe wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar ZEC wameelezea kutoridhishwa na maamuzi kadhaa yanayochukuliwa na Mwenyekiti wa Tume hiyo Jecha Salum Jecha ikiwemo yale ya kurudiwa kwa uchaguzi na kudai kwamba uamuzi huo haukuhusisha wajumbe wote wa ZEC.

Wakizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es salaam wajumbe hao wamedai kwamba ndani ya tume hiyo kumekuwepo kwa mgawanyiko wa viongozi kwa kile walichokieleza kwamba tume hiyo imeingiliwa na wanasiasa na hivyo kupelekea maamuzi yake mengi kuwa ni ya kisiasa.

Hata hivyo wameituhumu tume hiyo kukosa ushirikiano na wadau muhimu wa uchaguzi kutokana kuwepo na baadhi ya wanasiasa kususia uchaguzi na baadhi ya mashirika kukataa kuisaidia tume hiyo katika kufanikisha uchaguzi wa marudio.