Friday , 11th Mar , 2016

Tume ya Uchaguzi nchini Tanzania (NEC) imetakiwa kuruhusu wafungwa,wana vyuo pamoja na wagonjwa ili waweze kupata fursa ya kupiga kura na kutimiza haki yao ya msingi ya kidemokrasia.

Mwenyekiti mwenza wa SEMOT ,Martina Kabisama

Hayo yameelezwa na Wadau wa Masuala ya Uchaguzi katika mkutano wa Tathmini ya Uchaguzi mkuu uliofanyika Octoba mwaka jana ulioandaliwa na Mashirika binafsi ya SEMOT,TASEO na TEMCO, ambao ni waangalizi wa ndani wa uchaguzi ambapo wameishauri tume ya uchaguzi kufanya maboresho katika uandikishaji na upigaji kura ili kuyawezesha makundi yote kushiriki katika uchaguzi.

Waangalizi wa ndani wa Uchaguzi Rachel Maleza na Mwenyekiti mwenza wa Semot ,Martina Kabisama wamesema kuwa Changamoto kubwa waliyokutana nayo ni pamoja na kuzuiwa kuingia katika vituo vya kupiga kura hivyo kutofanya kazi yao kwa ufanisi jambo ambalo wameitaka tume kuangalia upya.

Dokta Alexandar Makulilo akitoa ripoti ya tathmini ya uchaguzi mkuu amesema kuwa kulikuwepo na vitendo vya rushwa katika kampeni pamoja na vitisho kutoka katika vyombo vya dola na vyama hasimu vya siasa

Baada ya kukusanywa kwa maoni mbalimbali kutoka kwa Wadau wa Uchaguzi,Ripoti Maalumu kuhusu tathmini ya Uchaguzi inatarajia kutoka hivi karibuni ikiwa na mapendekezo juu ya namna ya kuboresha chaguzi zijazo ili ziwe huru na za haki.