Friday , 11th Apr , 2014

Baadhi ya wafugaji nchini Tanzania wamedaiwa kukiuka taratibu za ufugaji kwa kuuza mazao ya mifugo yakiwemo mayai na nyama wakati mifugo yao ikiwa inapata matibabu.

Mtaalamu wa kilimo na mifugo kutoka kituo cha wakulima, Bw. Ali Abdallah Kitole, ameyasema hayo katika mahojiano na East Africa Radio, ambapo amekitaja kitendo hicho kuwa ni hatari kwa afya ya binadamu kutokana na nyama pamoja na mayai kuwa na kiwango kikubwa cha kemikali ambacho ni hatari kwa afya ya binadamu.

Kitole amefafanua kuwa kitaalamu kuna muda maalumu uliotengwa kwa mazao ya kilimo na mifugo kuanza kuliwa, ili kuruhusu sumu ya madawa itoke ndani ya mazao hayo, lakini kutokana na tamaa ya fedha za haraka baadhi ya wafugaji wamekuwa wakiuza mazao ya mifugo hata wakati wakitambua kuwa ni hatari kwa afya na maisha ya binadamu.