Friday , 11th Mar , 2016

Wachimbaji wadogo watano wamefariki dunia na wengine watatu kujeruhiwa baada ya kufunikwa na kifusi cha mchanga katika machimbo ya dhahabu katika kijiji cha Mgusu mkoani Geita.

Baadhi ya Wachimbaji wadogo wadogo wakiendelea na shughuli zao za kusaka Dhahabu katika eneo waliloachiwa wachimbaji hao eneo la Mgusu,wilayani Geita

Wakiongea mashuhuda wa tukio ambaoni ni wachimbaji wa mgodi huo wamesema kuwa ajali hiyo iliwakuta wachimbaji hao waliofunikwa na kifusi wakiwa wanajiandaa kulipua mwamba kwa ajili ya kutafuta madini.

Wiki moja kabla ya tukio hilo maafisa madini mkoa wa Geita walipiga marufuku kufanyika kwa shughuli zozote zile za uzalishaji kwenye eneo hilo kwa kuwa lilikua limeshaonyesha hali ya hatari ambapo wamesema wachimbaji hao walikuwa wanachimba kinyume cha taratibu na kufanya shughuli hiyo usiku.

Mganga mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Geita Adam sijaona, amethibitisha kupokea kwa maiti watano na majeruhi watatu ambao wamepewa rufaa ya kwenda hospitali ya rufaa ya Bungando iliyopo jijini Mwanza kwa matibabu zaidi baada ya hali zao kuwa mbaya.

Tukio hilo limetokea hivi karibuni baada ya wachimbaji hao wanane kuingia kuchimba kwenye eneo hilo linalomilikiwa na chama cha wachimbaji wadogo Mgusu lenye leseni 20 za uchimbaji.