Wednesday , 2nd Sep , 2015

Wachimbaji wadogo wa madini kutoka mikoa mbalimbali wamelalamikia uchimbaji wa kubahatisha walioufanya kwa kipindi kirefu na kuwasababishia hasara ikiwemo upotevu wa mitaji.

Rachel Njau ni Mchimbaji wa Madini ya Tanzanite

Wachimbaji hao wameiomba serikali iwasaidie kupata wataalamu wa miamba watakaowasaidia kufanya uchimbaji wa uhakika utakaowanufaisha kiuchumi na kuinua pato la taifa.

Wakizungumza katika jukwaa la wanawake wachimbaji lililoandaliwa na shirika lisilokuwa la kiserikali la Haki Madini lililofanyika mkoa wa Kilimanjaro, wanawake hao wamesema kuwa uchimbaji wa kubahatisha ni changamoto inayowakabili wachimbaji wengi huku wakikutana na wataalamu feki wa miamba.

Rachel Njau ni Mchimbaji wa madini ya Tanzanite ameiomba serikali kuchukua wasomi waliobobea katika masuala ya miamba na kuwaelekeza kwa wachimbaji ili waweze kuchimba kitaalamu na kupata faida.

Mwezeshaji wa wachimbaji wadogo kutoka mkoa wa Morogoro Martha Bitwale amesema kuwa wachimbaji wengi hawana uelewa juu ya madini na thamani yake hali inayowapelekea kudanganywa na wakati mwingine kudhulumiwa hivyo amewataka wachimbaji kujiendeleza kielimu ili kuondokana na kadhia hiyo.

Afisa madini Mkoa wa Kilimanjaro Fatma Kyando amesema kuwa Wizara ya madini kupitia Ofisi za mikoa na kanda zimekua na juhudi za kutoa elimu kwa wachimbaji ili waweze kuchimba kitaalamu na kuzingatia usalama wao wanapokua migodini.