Friday , 10th Apr , 2015

JESHI la polisi mkoani Mara limewaomba wananchi mkoani humo kutoa ushirikiano katika oparesheni ya kuwasaka watu wanaojihusisha na utengenezaji wa Noti bandia ambazo zimeingizwa katika mzunguko wa fedha na kununua bidhaa bila kutambulika.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Musoma, kamanda wa polisi mkoa wa Mara ACP Phillip Kallangi amesema kuwa kuna tetesi kuwa kuna fedha bandia zinazotumika mitaani bila wananchi kutambua na kuwataka wananchi kutoa taarifa kwa viongozi wa Serikali za mitaa ama polisi ili kudhibiti vitendo hivyo.

Kamanda Kalangi amesema Aprili 8 mwaka huu majira ya saa 5.20 mchana vijana wawili wamekamatwa wakiwa na noti bandia nne kila moja ikiwa na thamani ya 2000 hivyo zote kwa pamoja zikiwa na jumla ya 8000.

Amewataja vijana hao ambao wamekamatwa na noti hizo kuwa ni kuwa ni Bw John Ezekiel (19) mkazi wa mtaa wa Nyakato na Balimba Josephat (31) mkazi wa mtaa wa Baruti mjini Musoma ambapo kwa pamoja walikamatwa na fedha hizo katika baa ya GMC iliyopo kata ya Nyakato mjini humo.

Kamanda Kalangi amezitaja namba za noti hizo kuwa ni ck 1942902,ck 1942914,ck 1942915 na ck 1942924 na kwamba vijana hao wanaendelea kushikiliwa na polisi kwa mahojiano zaidi ili kubaini mtandao huo na kilipo kiwanda cha kutengeneza fedha hizo.