WAKAZI wa kijiji cha Chimati wilayani Butiama mkoani Mara wamekubwa na hofu kubwa baada kuibuka kundi la wanyama wakali aina Viboko ambao wamekuwa wakiwashambulia wavuvi katika eneo hilo na kusabisha mtu mmoja kufariki dunia huku wawili wakijeruhiwa vibaya.
Afisa mtendaji wa kijiji hicho Bw Benedicto Sonenga katika taarifa yake yenye kumbukumbu namba CMT/BT/VOL.01 kwenda kwa mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Musoma na nakala kuwasilishwa kwa kamanda wa polisi mkoa na mkuu wa mkoa Mara kwa ajili ya msaada,amesema hivi sasa kundi hilo la wanyama hao wakali limekuwa likiwashambulia wavuvi na kusababisha hofu kubwa kwa wananchi.
Katika taarifa hiyo afisa mtendaji huyo wa kijiji amesema kuwa usiku wa juzi wavuvi watatu wakiwa ndani ya mtumbwi katika eneo la kome katika ya ziwa Viktoria Viboko hao walivamia mtumbwi na kuanza kuwashambulia huku wakimng’ata mmoja wao Mtiti Magesa Masige na kutoa utumbo wake nje kabla ya kunyofoa sehemu zake za siri na kuondoka nazo na hivyo kusababisha kifo chake.
Kiongozi huyo wa kijiji amewataja walionusurika katika tukio hilo kuwa ni Bw Mugeta Magembe na Petro Matete wote wakazi wa kijiji cha Chimati huku akimuomba mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Musoma kuchukua hatua za haraka za kudhibiti wanyama hao hatari ambao amedai mbali na kuwa tishio kwa kushambulia wavuvi ndani ya ziwa hilo lakini pia wamekuwa wakivamia makazi ya wananchi na kuharibu pia mazao mbalimbali ya wananchi mashambani.