Sunday , 27th Mar , 2016

Uvuvi haramu wa kutumia sumu kali, pamoja na neti umekua ukitishia uhifadhi katika hifadhi ya taifa ya Saa Nane na Lubondo ambazo zimepewa jukumu la kulinda mazalia ya samaki ili samaki hao wasipotee kwenye uso wa dunia.

Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Saa nane Jijini Mwanza, Donatus Bayona

Akizungumza na Waandishi wa Habari Ofisini kwake waliofanya ziara ya kutembelea hifadhi hiyo ya Saa Nane iliyoko jijini Mwanza ziara iliyoratibiwa na Tanapa Mhifadhi Mkuu Donatus Bayona amesema kuwa changamoto inayowakabili ni uvuvi haramu na uvamizi wa maeneo ya hifadhi unaofanywa na wavuvi wanaojipatia kipato bila kujali kuwa wanaharibu mazalia ya samaki.

Mhifadhi huyo amesema kuwa hifadhi hiyo ambayo iko katikati ya jiji la Mwanza inaongoza kwa kuwa na watalii wengi wa ndani ambao ni asilimia 90% ya wageni wanaotembelea hifadhi hiyo.

Askari Wanyamapori katika hifadhi hiyo Aloyce Mong`ee amesema kuwa wamekuwa wakiimarisha doria katika mipaka ya hifadhi ili kuzuia shughuli hizo za uvuvi ambazo ni tishio kwa uhifadhi.

Hifadhi ya Saa Nane ni moja kati ya hifadhi zilizopo katikati ya miji hivyo kuvutia watanzania wengi kutembelea eneo hilo ambalo lina wanyama pori pundamilia, swala na sokwe weusi pamoja na mandhari nzuri na maridhawa ambazo hutumika kama sehemu ya kujifunzia na kupumzikia.