Wednesday , 26th Nov , 2014

Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi nchini Tanzania Mh. Dkt. Titus Kamani amesema matatizo yanayowakabili wafugaji na sekta ya Mifugo kwa ujumla ni matokeo ya utendaji kazi mbaya wa wataalam na wasomi wa fani hiyo.

Akizungumza wakati anafungua mkutano wa 32 wa mwaka wa wataalam wa mifugo unaofanyika Jijini Arusha Dkt. Kamani amesema wasomi wengi wa fani ya mifugo wametelekeza fani zao na kukimbilia fani zingine jambo linalosababisha wafugaji kuendelea kuteseka na mifugo.

Aidha Dkt. Kamani amesema kuanzia sasa wizara yake imeanza mchakato wa kuhakikisha kuwa wataalam wote wa fani ya mifugo wanaonesha mfano kwa vitendo kwa yale waliyosomea ikiwa ni pamoja na kuwa na mashamba ya mifugo ambayo yatawawezesha wafugaji kujifunza hatua itakayopunguza matatizo katika sekta hiyo.

kwa upande wao baadhi ya watalaam wamesema tatizo kubwa liko kwenye sera na kwamba kama hazitabadilishwa itakuwa vigumu kuleta mabadiliko katika sekta hiyo huku baadhi ya wafugaji wakiendelea kulalamikia kukithiri ahadi na matamko ya serikali ambayo asilimia kubwa yamekuwa hayatekelezwi.