Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Tanzania IGP Ernest Mangu.
Akizindua utafiti huo leo jijini Dar es Salaam, Mtafiti wa Twaweza Elvis Mushi amesema wananchi wanamsukumo zaidi wa kutoa rushwa hata wasipoombwa wakati wanatafuta huduma muhimu zikiwemo Maji, Elimu na Afya huku ikionekana kutoa rushwa ni jambo la kawaida kutoa na kuombwa mara kwa mara.
Kwa upande wao, Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu LHRC, Dkt. Helen Kijo-Bisimba amesema asilimia kubwa ya wananchi wanaamini rushwa haiwezi kumalizika kutokana na kutokuwa na mipango thabiti ya kuitokomeza.
Wakati huo huo, mtandao wa Wanafunzi nchini Tanzania (TSNP) umesema wanaokwamisha uundwaji wa Katiba mpya wanarudisha maendeleo ya nchi na kwamba mchakato huo haupo kwa ajili ya kuonesha misimamo ya kisiasa bali namna gani taifa litaongozwa na Katiba iliyotokana na mawazo yao.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Mtandao huo, Bw. Alphonce Lusako ambapo ameeleza kuwa endapo mchakato wa kupata katiba mpya utakwama itakuwa ni dhambi ya kihistoria ambayo haitaweza kufutika machoni pa watanzania.
Aidha, Lusako ameongeza kuwa kutofautiana ni demokrasia lakini demokrasia safi ni ile inayojenga muafaka, maridhiano na makubaliano na sio kubomoa na kuwataka wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba watambue sheria kuu ndani ya bunge hilo ni kuboresha Katiba ya wananchi.