
Picha haihusiani na tukio.
Akizungumza na www.eatv.tv, Mkurugenzi wa huduma za utabiri TMA, Dkt. Hamza Kabelwa amesema upepo huo umetokana na kuimarika kwa hali ya hewa kwenye eneo la Kusini Mashariki mwa bara la Afrika na mfumo wa upepo wa kusini.
Dkt. Kabelwa amewataka wananchi pamoja na mamlaka zinazoshughlika na usafiri wa majini kuwa makini kwa kuchukua tahadhari kuhakikisha hakuna maafa yanayoweza kutokea.
"Upepo huo mkali utavuma kwa siku tatu kwenye Ukanda wa Pwani ya bahari ya Hindi na maziwa yote makuu likiwemo ziwa Nyasa, Viktoria na Tanganyika na mikoa yote iliyopakana na maeneo hayo, ambayo ni mikoa ya kanda ya kati, tunaendelea kufuatilia mwenendo wa upepo huo na kutoa tahadhari kila inapolazimika kufanya hivyo", amesema Dkt. Kabelwa.
Kufuatia tahadhari hiyo tayari baadhi ya kampuni zinazojihusisha na usafirishaji wa majini, zimesimamisha huduma kutokana na tahadhari ya kuwepo kwa upepo huo.