Namna ya kupata huduma inayotolewa na mfumo huo mpya wa usafiri wa teksi maeneo ya mijini.
Kupitia simu za mkononi, mteja anaweza kuwasiliana na taksi iliyo karibu yake huku akipata maelezo yote muhimu kama vile jina, sura, namba pamoja na aina ya gari, huku pia dereva akiwa na uwezo wa kupata maelezo yote muhimu kuhusu mteja anayewasiliana nae.
Huduma hiyo inatumika katika miji zaidi ya 470 kwenye mataifa mbali mbali ulimwenguni ambapo kwa upande wa Afrika Mashariki, Kenya ndio nchi ya kwanza kuanza kutumia huduma hiyo ikifuatiwa na Tanzania.
Hata hiyo kumekuwa na maoni hasi kutoka kwa wamiliki na madereva taksi nchini ambao katika mahojiano na EATV wameitaka serikali kuitathmini huduma hiyo na athari zake kwa biashara ya usafiri wa teksi.
"Mimi kwa kweli siungi mkono mfumo huu wa usafiri kwani haujulikani gari ipi ni taksi na ipi sio taksi maana hata gari binafsi zinaruhusiwa kubeba abiria tofauti na sasa ambapo taksi tena zenye utambulisho maalumu ndiyo zinaruhusiwa," amesema dereva teksi Mgeni Saidi.
Dereva mwingine Selemani Khalfani amesema uwepo wa mfumo huo utaongeza ugumu wa biashara ya usafirishaji kwa njia ya teksi kwani hadi sasa uwepo wa bodaboda, bajaj na mabasi mwendokasi pekee vimekuwa sababu ya kudorora kwa biashara ya usafiri wa teksi.