Tuesday , 13th May , 2014

Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), limezitaka serikali katika nchi mbalimbali duniani kuhakikisha zinalinda maliasili za misitu hasa zile zilizo katika hatari ya kutoweka.

Mkuu wa utawala wa shirika la maendeleo la umoja wa mataifa UNDP, Bi. Helen Clarke.

Wito huo umetolewa leo Jijini Dar es Salaam leo na Mkuu wa Utawala wa UNDP, Bi. Hellen Clarke, wakati wa mkutano wake na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam katika siku yake ya nne na ya mwisho ya ziara yake ya kikazi nchini.

Kwa mujibu wa Bi. Clarke, maliasili zilizo katika hatari ya kutoweka ni pamoja na wanyama jamii ya tembo na faru ambao kimsingi amesema kutoweka kwao kunatokana na wimbi la ujangili na uwindaji haramu unaofanyika katika nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania.

Kauli ya Bi. Clarke imekuja wakati ambapo serikali ya Tanzania imekuwa ikiendesha kampeni ya kukabiliana na ujangili hususani wa wanyama jamii ya tembo, ambapo yeye mwenyewe ameunga mkono kampeni hiyo
kwa maelezo kuwa alishawahi kuendesha kampeni kama hiyo wakati alipokuwa waziri anayehusika na maliasili katika serikali ya Australia ambako anatoka.