Wednesday , 13th Dec , 2017

Unga wa muhogo umeelezwa kuwa na matumizi mbalimbali, zaidi ya kupikia ugali pia hutumika kutengeza Kibiriti ambapo unga huo hutengeneza kile kishungi cha kuwashia moto kinachokaa mbele ya kijiti cha kibiriti.

Hilo limethibitishwa na Mkurugenzi wa Kiwanda cha kusaga muhogo cha Ukaya, Mkuranga, Mkoani Pwani, Ibrahim, mbele ya uongozi wa Mtandao wa Kijani Kibichi Tanzania (Mkikita) uliotembelea kiwanda hicho.

Akiongea na uongozi wa Mkikita Ibrahim amesema kuwa miongoni mwa wateja wakubwa wa unga wao ni viwanda vya kutengenezea Vibiriti ambavyo vinautumia kwa kutengenezea kishungi cha njiti ya kibiriti kinachotumika kuwasha moto.

“Unga wetu wa muhogo tunaosaga hapa una wateja wengi sana kutokana na matumizi mbalimbali ambayo unaweza kufanya, ukitoa wateja kwaajili ya chakula, lakini Unga wa muhogo hununuliwa sana viwanda vya kutengeneza Kibiriti kwasababu hutumika kutengeneza kile kishungi cha kuwashia moto”, ameeleza Ibrahim.

Mbali na kupikia ugali na kutengeneza kishungi cha Kibiriti Ibrahim amebainisha kuwa Unga huo pia hutumika kutengenezea dawa ya kuzuia kuhara, Pombe, Mafuta pamoja na chakula cha wanyama.