Sunday , 28th Feb , 2016

Umoja wa Afrika kupitia kwa rais wa Afrika Kusini Bw. Jacob Zuma, umesema utatuma nchini Burundi waangalizi mia moja wa haki za kibinaadamu pamoja na idadi kama hiyo ya waangalizi wa kijeshi.

Akizungumza mara baada ya kumaliza ziara ya siku mbili akiwa kama kiongozi wa ujumbe wa viongozi watano waliotumwa na Umoja wa Afrika nchini humo; Rais Zuma amesema Rais Pierre Nkurunziza amekubaliana na mpango huo unaolenga kumaliza machafuko ya kisiasa nchini Burundi.

Ujumbe wa Afrika nchini Burundi umejumuisha Marais Jacob Zuma wa Afrika Kusini, Macky Sall wa Senegal, Muhammed Ould Abdul Aziz wa Mauritania, Ali Bongo wa Gabon na Waziri Mkuu wa Ethiopia, Hailemariam Desalegn. Hata hivyo Rais huyo wa Afrika Kusini hakusema ni lini waangalizi hao watawasili nchini Burundi.

Safari ya siku mbili ya ujumbe wa Umoja wa Afrika nchini Burundi imetajwa ni juhudi za umoja huo za kujaribu kuhitimisha mgogoro wa nchi hiyo baada ya serikali ya Rais Pierre Nkurunziza kupinga kupelekwa kikosi cha kusimamia amani nchini humo. Licha ya ujumbe huo kueleza kuwa, safari hiyo ilikuwa na mafanikio, mrengo wa upinzani nchini Burundi umetangaza kuwa, hauna matumaini na natija nzuri ya mazungumzo hayo.

Burundi ilitumbikia katika machafuko ya ndani mwishoni mwa mwezi Aprili mwaka jana baada ya kiongozi wa sasa wa nchi hiyo Pierre Nkurunziza kutangaza nia yake ya kugombea nafasi hiyo kwa mara ya tatu mfululizo. Hadi sasa mamia ya watu wameuawa katika machafuko hayo na maelfu ya wengine wamelazimika kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi hiyo.