Umati wa wakazi wa jiji la Mwanza, leo wamefurika kwa wingi katika uwanja wa ndege wa Mwanza na ukumbi wa Gandh kwa ajili ya kumpokea waziri mkuu wa zamani Edward Lowassa, wakati alipowasili kuanza safari ya matumaini ya kusaka wadhamini.
Katika safari yake hiyo kwa ajili ya mikoa 12 ya Tanzania Bara na mitatu visiwani, maelfu ya wanachama wa chama cha mapinduzi (CCM) wamejitokeza kumdhamini katika wilaya za Nyamagana na Ilemela.
Akiwa wilayani Nyamagana, Lowassa amefanikiwa kupata jumla ya wadhamini 3,127 huku wilaya ya nyamagana wakipatikana 1,671 na ilemela wadhamini 1,456.
Awali alipowasili katika jiji la Mwanza, Lowassa alipokelewa na umati mkubwa wa wakazi wa jiji la Mwanza kuanzia misafara ya pikipiki, magari na watembea kwa miguu.
Akitangaza wadhamini waliomdhamini mgombea huyo, katibu wa CCM wilaya ya Nyamagana, Elias Mpanda, katika mkutano uliofanyika ukumbi wa Gandh jijini humo, amesema wadhamini hao wamepatikana wilayani hapo kutokana na kuamua kuchukua maamuzi ya kumkubali na kuamini kiongozi huyo ni mtendaji mzuri wa kazi.
Katika wilaya ya Ilemela, katibu wa CCM wa wilaya hiyo, ole Meliuti, amesema wanachama hao wamejitokeza kumdhamini Lowassa kutokana na matumaini waliyonayo endapo atapata nafasi ya urais atakuwa muarobaini wa matatizo yao.
Naye mwenyekiti wa CCM mkoa wa shinyanga, Khamis Mgeja, amesema Lowassa amekuwa wa kwanza kuingia mkoa wa Mwanza kutokana na kuwa kitovu cha mikoa ya kanda ya ziwa.
Mgeja amesema ngome kubwa ya Lowassa ipo mikoa ya kanda ya ziwa, hivyo ni kiongozi ambaye ataweza kutatua changamoto iwapo atafanikiwa kushinda nafasi hiyo.
Naye mwakilishi wa wazee mkoa wa Mwanza, Emmanuel Lutalaka, amesema kiongozi lazima aandaliwe na awe mchapakazi.
Alisema anapochaguliwa Rais pia anachaguliwa mwenyekiti wa chama, hivyo wachague mtu ambaye anakijua chama na mwenye uchungu na chama hicho.
Aidha, Lowassa amesema mtaji wa mwanasiasa yeyote ni watu, hivyo kutokana na mapokezi makubwa aliyoyapata Mwanza, ana imani uchaguzi wa mwaka huu utakuwa mzuri zaidi.
“Watanzania watafakari nchi yetu kwa sasa imepata gesi, hivyo gesi hiyo inaweza kututajirisha ama kutufukarisha kulikoa kuyaacha mataifa makubwa yanaweza kuvuna na kutunyonya maana gesi ni laana ama baraka kwetu”, amsema Lowassa