Tuesday , 29th Sep , 2015

Mkutano wa kampeni ya mgombea urais kupitia chama CHADEMA, Edward Lowassa umeahirishwa mara baada ya wananchi kujitokeza kwa wingi kumsikiliza hali iliyopelekea baadhi ya wananchi kupoteza fahamu kwa kukanyagana uwanja wa Tangamano jijini Tanga.

Kampeni za mgombea urais kupitia UKAWA akiwa amezungukwa na Umati wa Watu jana Jijini Tanga ambapo mkutano wake Uliahirisha kutokana na msongamano

Wananchi hao walijitokeza kwa wingi kwa ajili ya kuonyesha nia ya kuhitaji mabadiliko na kumkubali Lowassa kuiongoza Nchi kwa madai kuwa wamechoshwa na sera za Chama Cha Mapinduzi CCM za ahadi zisizotekelezeka.

Sambamba na hayo baada ya mkutano huo kuahirishwa wananchi waligoma kuondoka katika viwanja hivyo kutokana na kuhitaji Lowassa ahutubie hali iliyomlazimu mgombea huyo kuzungumza na wananchi kwa muda mfupi na kuwaahidi wananchi kuwa hatowaangusha endapo atapata ridhaa ya kuiongoza nchi atahakikisha anapambana na umasikini pamoja na kufanya mabadiliko katika kila sekta.

Aidha ameongeza kuwa kama atapata ridhaa ya kuiongoza nchi atahakikisha ndani ya miezi tisa ya mwanzo anafufua bandari ili iweze kufanya kazi kwa masaa yote tofauti na inavyofanya kazi sasa pamoja na reli ya kutoka Tanga mpaka Musoma mkoani Mara kupitia Arusha.

Kwa upande wake waziri mkuu mstaafu Fredrick Sumaye amewaomba wakazi wa mkoa wa Tanga kumpa kura za ndio Lowassa katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu na kuachana na ahadi zisizotekelezeka.