Monday , 30th Nov , 2015

Wanazuoni wa Afrika wamesema umasikini wa nchi za Afrika ikiwemo Tanzania unatokana na ukosefu wa utawala bora na sio rasilimali.

Mkurugenzi wa Kituo cha Maendeleo Dkt. Suma Kaare

Kwa kuzingatia changamoto hiyo taasisi za kitaaluma na vyuo vimetakiwa kubuni mbinu mbadala za ufundishaji, ili kuzijengea uwezo asasi za kijamii na watumishi katika ngazi za umma na binafsi, kuweza kuwashirikisha wananchi katika mipango yao ya maendeleo.

Katika kituo cha maendeleo cha kimataifa ambacho kinaendeshwa kwa ushirikiano baina ya nchi za Tanzania na Denmark kilichopo USA RIVER nje kidogo ya jiji la Arusha kimesema kimekuwa kikitoa mafunzo maalumu kwa viongozi wa kada mbalimbali ili kuwajenga katika misingi ya kujali utawala bora na maendeleo ya wananchi.

Mkurugenzi wa kituo hicho Dkt Suma Kaare, amebainisha hayo wakati wa kuhitimishwa kwa mafunzo katika kozi za shahada ya sanaa katika masomo ya maendeleo na stashahada ya uongozi na utawala bora kituoni hapo.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Arumeru, Wilson Nkhambaku, aliyehudhuria hafla hiyo amesema masomo ya utawala bora na maendeleo yanayofundishwa kituoni hapo yatajenga jamii itakayoogopa rushwa na ufisadi.

Baadhi ya viongozi wa sekta binafsi na za umma kutoka mataifa mbalimbali wakiwemo wabunge kutoka nchi mbalimbali wamesema viongozi wa Afrika wanahitaji mtazamo mpya wa namna ya kuwahudumia watu wao na kuwaletea maendeleo.

Kozi hiyo ilikuwa ikiendeshwa na kituo cha MS-TCDC kwa ushirikiano na Kituo cha Maendeleo ya Masomo cha Kimmage cha nchini Ireland (KDSC) ambapo jumla ya wahitimu 18 wa shahada na sita wa stashahada kutoka nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Sudan Kusini, Zambia, Ehiopia na Ujerumani walitunukiwa vyeti vyao.