Kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro Ulrich Matei,
Mkazi wa kitongoji cha Mgudeni kijiji cha Dumila,Mkoani Morogoro,Bi.Pendo Mwafiyanga, anashikiliwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za kumfanyika ukatili mdogo wake kwa kumpiga na kumchoma na pasi katika maeneo mbalimbali ya mwili wake.
Mwanamke huyo ambaye amekuwa akiishi na mdogo wake huyo ambaye ni mtoto wa mama yake mkubwa anadaiwa kumfanyia ukatili kwa kumpiga na chupa ,kumfinya kwa mikasi,kumchoma kwa pasi ,kumkanyaga mwilini pamoja na kumfanyisha kazi ngumu zikiwemo kumbebesha madumu makubwa ya maji.
East Africa Radio imefika hadi katika kijijini cha Dumila na kuzungumza na Mtoto Mwamboli mwenye umri wa miaka nane ambapo anaeleza namna dada yake alivyokuwa akimfanyia ukatili huku mpangaji wa nyumba wanayoishi akieleza namna walivyokuwa wakishuhudia unyanyasaji huo.
Kwa Upande wake mama mwenye nyumba wanayoishi motto huyo amesema baada ya kuona matukio ya ukatili dhidi ya mtoto walichukua hatua ya kumkalisha kikao lakini alitoa majibu mabaya huku akiendelea na tabia hiyo hali iliyopelekea kutoa taarifa kwa mwenyekiti wa kitongoji naye kuzungumza na mwanamke huyo bila mafanikio.
East Africa Radio imefika katika kituo cha Afya Dumila na kuzungumza na afisa tabibu mfawidhi wa kituo hicho Dokta Mathew Kiyungu ambapo amesema alipata taarifa za mtoto huyo kufikishwa kwenye kituo hicho na kwamba walibaini majeraha sehemu mbalimbali za mwili wa mtoto na kisha kumpatia matibabu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro Ulrich Matei, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kujibu mashitaka yanayomkabili.