Mkuu wa Polisi nchini Tanzania IGP Ernest Mangu.
Akiongea leo jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa umoja huo ambaye pia ni Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Namibia IGP Sebastian Ndeitunga amesema SAPCCO imejipanga kukabiliana na uhalifu wa aina zote ikiwa ni pamoja na tishio la ugaidi katika ukanda huo huku ushiriki hafifu wa wananchi katika kukabiliana na uhalifu ukichangia kuongezeka kwa vitendo hivyo hali inayohitaji nguvu ya pamoja ili kukabiliana na uhalifu.
Kwa upande wake Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Tanzania, IGP Ernest Mangu akizuingumzia milipuko ya mabomu iliyotokea jijini Arusha amesema wanaendelea kufanya uchunguzi ili kuwabaini waliohusika huku akiwataka wananchi kushiriki kikamilifu katika kulisaidia jeshi la polisi kwa kutoa taarifa mara wanapohisi kuna dalili za kutokea kwa uhalifu.
IGP Mangu amesema bado jeshi hilo halifahamu hasa ni kwa nini matukio mengi ya milipuko hutokea katika miji ya kitalii ya Arusha na Zanzibar na kwamba kwa sasa wanazifanyia kazi taarifa za kiitelijensia kuhusiana na wahusika wa milipuko hiyo.