Sunday , 17th Apr , 2016

Wakulima wa zao la korosho nchini wametahadharishwa juu ya uwepo wa ugonjwa wa mnyauko ambao unatajwa kuwa ni hatari zaidi katika kuua mikorosho kwa kipindi kifupi mara baada ya kupata maambukizi.

Hadhari hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Mfaume Juma, wakati wa utambulisho wa ugonjwa huo kwa waandishi wa habari ambao kwa kutumia vyombo vyao wakulima watapata fursa ya kuufahamu ugonjwa na kujua dalili zake.

Kutokana na ugonjwa huo kuenezwa na vimelea aina ya Uyoga vinavyojulikana kama Fusarium Oxysporum vinavyojificha katika udongo wa mikorosho iliyoathirika, Mkurugenzi huyo amewataka wakulima kusafisha majembe yao baada ya kuyatumia pamoja na kutopanda miche kutoka katika mashamba mengine.

Kwa upande wake, Mtafiti Mstaafu kutoka katika Taasisi ya Utafiti wa Kilimo ya Naliendele, Dk. Shamte Shomari, amezitaja baadhi ya dalili za ugonjwa huo kuwa ni pamoja na mjani katika baadhi ya matawi ya mkorosho kupoteza rangi yake ya kawaida ya kijani na kubadilika kuwa njano na baadaye kuwa kahawia.

Sauti ya Dk. Shamte Shomari,
Sauti ya Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Mfaume Juma