Wanafunzi wa Chuo Cha Sayansi Ya Jamii Na Lugha Katika Chuo Kikuu Cha Dodoma Wakiandamana Kuelekea ofisini Kwa waziri Mkuu Mjini Dodoma.
Akizungumza na waandishi wa habari jana chuoni hapo waziri wa mikopo wa kitivo cha elimu, Mpandalume Saimon alisema fedha hizo hazijaingizwa takribani miezi mitatu suala linalowafanya wanafunzi wa chuo hicho kuishi maisha magumu.
Amesema hali imekuwa mbaya kwani kuna baadhi ya wanafunzi mpaka sasa hawana fedha za kununulia chakula pamoja na matibabu hali inayowafanya wengi wao kuishi maisha magumu chuoni hapo.
Amesema Tumepata habari kuwa fedha zimeshaingia kwenye akaunti ya chuo lakini mpaka sasa ninavyozungumza na nyie ni kwamba hakuna mwanafunzi hata mmoj aambaye ameshaingiziwa fedha za kujikimu kwenye akaunt yake.
Amesema hawataingia madarasani hadi hapo serikali itakapoingiza fedha zao za kujikimu kwenye akaunti zao.
Wanafunzi hao wamesisitiza kuwa hawataingia madarasani hadi hapo Waziri Mkuu Mizengo Pinda atakapofika chuoni hapo na kuzungumza nao kwani wamekuwa wakipewa ahadi zisizo tekelezeka.
Kwa kuthibitisha hilo wanafunzi hao walikataa kuongea na ujumbe uliotumwa na waziri mkuu kwa ajili ya kuzungumza nao na kuweka mambo sawa.
Wajumbe hao walikuwa ni mkuu wa mkoa wa Dodoma, Chiku Gallawa, kaimu mkuu wa wilaya ya Dodoma, Farida Mgomi na waziri wa afya na ustawi wa Jamii, Dk, Kebwe Steven Kebwe ambapo wanafunzi hao walikataa katakata kuzungumza nao kwa madai kuwa wanamtaka waziri mkuu mwenyewe aje wazungumze nae.
Kwa upande wake Rais wa serikali ya wanafunzi wa UDOM Fredrick Lutelano amesema hakuna mgomo wala maandamano katika chuo.
Hata alipoelezwa na mwandishi kuwa yuko kwenye maandamano ya wanafunzi amesema kuwa hayo maandamano yamekwisha na kila kitu kimekaa sawa japo alikiri kuwa fedha za wanafunzi hao za kujikimu bado hazijafika.