Thursday , 28th May , 2015

Zoezi la kuandikisha wananchi kwenye daftari la kudumu la wapiga kura katika Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma limeendelea, ambapo idadi ndogo ya wananchi imejitokeza katika zoezi hilo.

Mchambuzi Mwandamizi wa Compyuta wa Tume ya Uchaguzi ya Taifa, Frank Mhando akimuonyesha Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Chiku Gallawa moja ya mashine ya BVR

East Africa Raido imetembelea kwenye baadhi ya vituo vya kujiandikishia vilivyopo katika vijiji vya Fufu na Suli na kukutana na idadi ndogo ya wananchi wanaojiandikisha katika daftari hilo ambapo katika kituo cha Shule ya Masingi ya Fufu kulikuwa na mwananchi mmoja tu aliyekuwa anajiandikisha na hapakuwa na foleni ya watu.

Hata hivyo msimamizi wa kituo hicho, Emmanuel Chidong’oi amesema kuwa kumekuwa na mwitikio mdogo kwa wananchi wa kijiji hicho kujitokeza kujiandikisha hali iliyowafanya kutotimiza malengo yao waliyojiwekea ya kuandikisha wananchi 600.
Amesema mpaka jana walikuwa wameandikisha watu 419 tu ambapo ndiyo ilikuwa siku ya mwisho ya kujiandikisha.

Kwa upande wa kituo cha kuandikishia wapiga kura cha shule ya msingi Sule pia kulikuwa na idadi ndogo ya wapiga kura hali iliyoelezwa na msimazi wa kituo hicho Anna Maghembe kuwa idadi ya wapiga kura waliyokuwa wamejiwekea ilikuwa imetimia kwani walikuwa wamejipangia kuandikisha wapiga kura lakini mpaka jana walikuwa wameandikisha watu 359.

Aidha katika vituo hivyo mashine za BVR zilikuwa zinafanya kazi kwa kasi kwani mtu mmoja alikuwa anatumia dakika 2 tangu kuchukuliwa taarifa zake muhimu za kuingizwa kwenye daftari hilo hadi kupewa kitambulisho chake.

Katika hatua nyingine mwenyekiti wa kitongoji cha Teya kilichopo katika kata ya Ilindi Wilayani Bahi, Njeti Nyambura, ameiomba NEC kukiongezea kitongoji hicho muda wa kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura.

Amesema hiyo inatokana na zoezi hilo kutofanyika kwa ufasaha siku ya kwanza baada ya mashine hizo kushindwa kufanya kazi na kuwalazimu wananchi kuanza kujiandikisha majira ya saa kumi jioni.

Amesema kuwa walikuwa wamejiwekea lengo la kuandikisha wapiga kura 2,000 lakini mpaka jana walikuwa wameandikisha watu 369 tu na kituo katika kitongoji chote kipo kimoja tu hivyo kuiomba NEC kuwaongezea muda kidogo ili waweze kutimiza lengo kwani tumebakiwa na siku moja tu ya kujiandikisha ambayo ni leo