Friday , 29th May , 2015

Waziri mkuu wa Tanzania Mhe. Mizengo Pinda amewataka vyama vya utetezi wa kisheria nchini kushirikiana na serikali katika kutoa elimu kwa jamii ya kuondokana na mauaji ya watu wenye albinism pamoja na mauaji wa vikongwe yaliyokithiri.

Waziri mkuu wa Tanzania Mhe.Mizengo Pinda .

Akizungumza katika maadhimisho ya miaka 25 ya chama cha wanasheria wanawake nchini TAWLA, Mhe. Pinda amesema kati ya mwaka 2006 na 2015 watu wenye albinism 43 wamepoteza maisha pamoja na Wazee vikongwe zaidi ya 2200 wameuawa kutokana na imani za kishirikina pamoja na mila potofu.

Waziri Pinda amesema kuwa zipo kesi zinazoendelea kufuatia mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi pamoja na wengine kujeruhiwa huku waathirika wakubwa wakiwa ni wanawake na watoto hivyo amezitaka taasisi zinazotoa msaada wa sheria kusaidia utetezi wa makundi hayo ili haki itendeke.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa chama cha wanasheria wanawake nchini Tanzania TAWLA, Aisha Bade wanasema wameweza kuwafikia idadi kubwa ya wanawake wanaohitaji msaada wa kisheria nchini huku wakiongeza juhudi mbalimbali za msaada ikiwa ni pamoja na katika mikoa ya Simiyu, Geita na Mwanza yenye idadi kubwa ya mauaji ya vikongwe.