Thursday , 18th Dec , 2014

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka amegoma kujiuzulu kwakuwa haoni sababu ya kufanya hivyo

Prof. Anna Tibaijuka

Waziri Tibaijuka ambaye ni mmoja wa waliohusishwa na wizi wa fedha katika akaunt ya Escrow amesema hawezi kujiuzulu na wala hana mpango wa kufanya hivyo kwa kuwa fedha alizopewa na ndugu James Rugemalira zilikuwa za msaada wa shule na si vinginevyo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Profesa Tibaijuka amesema hawezi kujiuzulu na haoni sababu ya kufanya hivyo kwa kuwa fedha hizo alipewa kama ambavyo watu wengine walivyompa kama msaada wa shule na hakuona sababu ya kufuatilia kama fedha hizo zilikuwa za wizi ama la, licha ya kukiri hata yeye kiasi alichokikuta benki kwenye akaunti yake mara baada ya kutakiwa kufungua akaunti katika benki ya Mkombozi kuwa kikubwa.

Hata hivyo Profesa Tibaijuka amesema kwasasa anasubiri uchunguzi unaoendelea kufanyika na vyombo vilivyoteuliwa na atakapobainika kuwa fedha hizo alizipokea kimakosa au kwa njia ya wizi atakuwa tayari kuwajibika licha ya kukiri kuwa sheria ya maadili ya viongozi nchini, hairuhusu mtumishi yeyote wa serikali kupokea fedha zaidi ya 50,000 kama zawadi kutoka kwa mtu ua kikundi au tasisi.