Thursday , 16th Apr , 2015

Serikali imetakiwa kutoa taarifa ya utafiti kuhusiana na mafuta ya ubuyu ili kama hakuna uthibitisho wa madhara ya magonjwa yanayotokana na mafuta hayo basi wananchi waruhusiwe kuendesha biashara ya mafuta hayo bila matatizo yoyote.

Kiongozi mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe.

Wito huo umetolewa jana na kiongozi mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya mashujaa mjini Dodoma.

Amesema kwa kipindi cha miaka miwili sasa mamlaka ya chakula na dawa nchini (TFDA) ilifungia matumizi ya mafuta ya ubuyu kwa madai kuwa yana madhara kwa afya ya binadamu.

Aidha Mh. Zitto ameongeza kuwa uchumi wa watu wa dodoma umesimama na wengi wakiwa wamekumbwa na lindi la umasikini kutokana na kusimama kufanya shughuli za uzalishaji wa mafuta hayo ambayo kwa mujibu wa uchunguzi wa awali yanadaiwa kuwa na Madhara.

Zitto ametaka serikali ichukue hatua za haraka katika kuimalisha utafiti huo ili kuweza kuwakomboa wananchi wa mkoa wa Dodoma na pia kuliingizia taifa pato kutokana na biashara hiyo ya mafuta ya Ubuyu.

Kwa upande wake mwenyekiti wa chama hicho, Anna Mghwira amesema kuwa mkoa wa Dodoma siyo maskini kwani una rasilimali nyingi ambazo zikitumiwa ipasavyo zinaweza kuongeza pato la mwananchi wa mkoa huu na kuondokana na umaskini uliopo.