Friday , 13th Nov , 2015

Tanzania imeunga mkono mapendekezo ya kufanyia marekebisho Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ili liweze kufanya kazi ipasavyo, liwe jumuishi zaidi na ili lioane vyema na hali halisi iliyopo duniani sasa.

Balozi Ramadhan Mwinyi Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa.

Moja ya pendekezo iliyounga mkono ni mkakati wa Ufaransa na Mexico kuhusu matumizi ya kura ya turufu, kwamba isitumiwe katika masuala yanayohusu uhalifu wa mauaji ya halaiki na uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Akihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa leo wakati likikutana kuhusu kuboresha kazi ya Baraza la Usalama, Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania Balozi Ramadhan Mwinyi amesema wanachama wa Baraza la Usalama, hususan wenye nguvu za kura ya turufu, wanapaswa tu kuchukua hatua zinazoendana na dhamira na kanuni za Umoja wa Mataifa.

"Tunatoa wito kwa Baraza lijumuishe katika ripoti zake za siku za usoni kwa Baraza Kuu, tathmini ya hatua zilizochukuliwa na ambazo hazikuchukuliwa, zikiwemo kwa sababu ya matumizi ya kura ya turufu, pamoja na madhara yake. Imesisitizwa mara nyingi, na hata ujumbe wangu, kwamba ripoti ya Baraza la Usalama kila mwaka iwe yenye uchambuzi zaidi na ya kina." Amesema balozi Mwinyi.

Aidha, balozi Mwinyi amesema Tanzania inakaribisha hatua zinazochukuliwa ili kuongeza uwazi na ufanisi wa Baraza la Usalama, ikiwemo mijadala ya wazi ambayo Tanzania imekuwa ikishiriki.