Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto nchini Tanzania Bi. Sophia Simba.
Akizungumza jijini Dar es Salaam katika hafla ya uzinduzi wa kampeni ya kudhibiti ndoa za utotoni, Waziri wa maendeleo ya jamii, jinsia na watoto, Bi. Sofia Simba amesema Serikali kwa kushirikiana na mashirika ya Umoja wa Mataifa na wadau wengine wa maendeleo watatazama vyanzo vya ndoa za utotoni kuanzia kwenye masuala ya kiuchumi, kijamii, mila na desturi ili kuweza kulitokomeza suala hilo.
Hata hivyo baadhi ya wadau wakiongea na East Africa Radio wamesema suala la ndoa za utotoni sio suala la kuachia mashirika na serikali pekee na kwamba endapo wananchi watatoa taarifa katika vyombo husika tunaweza kuondoa tatizo la ndoa za utotoni kwa wasichana Tanzania.
Wakati huo huo, jamii imetakiwa kushiriki kikamilifu katika kupiga vita usafirishaji haramu wa binaadamu kuanzia katika ngazi ya familia kwa kuwa kwa sasa usafirishaji huo umekuwa ukiongezeka kwa kasi jambo linaloweza kuathiri nguvu kazi ya taifa .
Wakili Jemsi Marenga kutoka kituo cha masaada wa sheria cha NOLA,amesema hayo katika maafunzo maalumu kwa waandishi wa habari wa mkoa wa Arusha kuhusu namna ya kupinga usafirishaji haramu wa binaadamu,ambapo amesema usarishaji huo umeshamiri zaidi kwa watoto kutoka mikoani.
Baadhi ya washiriki wamesema biashara haramu ya binaadamu ni zama mpya hivyo kupitia mafunzo hayo waandishi walioshiriki wametambua viashiria vya usafirishaji huo jambo litakalosaidia kuwabaini wasafirishaji katika hatua za awali.