Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Zuberi Kabwe, amesema hayo leo ambapo amelitaka shirika la fedha la kimataifa IMF kufafanua ni kwa namna gani litazuia upotevu huo wa kiasi kikubwa cha pesa unaofanywa kupitia udhaifu uliopo kwenye mfumo wa kodi wa kimataifa.
Akizungumza wakati wa utoaji wa ripoti ya hali ya uchumi kwa nchi zilizo kusini mwa Jangwa la Sahara, Kabwe amesema inasikitisha kuona IMF imekuwa haichukui hatua za msingi kubadili hali hiyo kwani mara zote imekuwa ikiwakumbatia wawekezaji pamoja na makampuni makubwa.
Kwa mujibu wa Kabwe, nchi maskini ndio wahanga wa mfumo huo mbaya wa kodi, kwani wawekezaji na makampuni ya kigeni yamekuwa yakitumia udhaifu uliopo kwenye mfumo huo kwa kutoa taarifa zisizo sahihi kuhusu kiwango na mahali walikolipa kodi hiyo.
Aidha, kuhusu ripoti ya hali ya uchumi, IMF imesema uchumi wa nchi zilizo kusini mwa Jangwa la Sahara umekuwa kwa kasi ya kuridhisha ya wastani wa asilimia Sita na kwamba ukuaji huo uko mashakani kutokana na tishio la ugonjwa wa Ebola pamoja vita kwenye maeneo machache ikiwemo Jamhuri ya Afrika ya Kati pamoja na Sudani Kusini.