Friday , 20th Mar , 2015

MAELEZO BINAFSI YA MHE. ZITTO ZUBEIR KABWE, MB KUHUSU UANACHAMA WAKE KATIKA CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA) NA HATMA YAKE KAMA MBUNGE KATIKA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA.

Zitto Kabwe

DODOMA, ALHAMISI 19 MACHI 2015.
____________________________________
1) Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana kwa fursa uliyonipa kutoa maelezo yangu binafsi katika Bunge lako Tukufu leo. Ninatoa maelezo haya kwa mujibu wa Kifungu cha 50 (1) cha Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Aprili, 2013 kinachosema kwamba,

“Mbunge yeyote anaweza, kwa idhini ya Spika, kutoa maelezo binafsi Bungeni yanayolenga kufafanua kuhusu jambo lolote linalomhusu na lililoifikia jamii”

2) Mheshimiwa Spika, Nilijiunga na Bunge lako Tukufu kwa mara ya kwanza Mwaka 2015 nikiwa na lengo kuu la kupaza sauti ya vijana kwenye masuala yanayohusu nchi yetu na kutetea maslahi ya Watanzania hususani Wananchi wa Jimbo la Kigoma Kaskazini na Mkoa wa Kigoma, na Watanzania kwa ujumla. Nilichaguliwa na wananchi wa Kigoma Kaskazini kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA). Wananchi wa Kigoma Kaskazini walinichagua tena Mwaka 2010 kupitia tiketi ya CHADEMA.

3) Mheshimiwa Spika, kupitia fursa ya ubunge niliyopewa na wananchi wa Kigoma Kaskazini kwa udhamini wa CHADEMA, nimejifunza mengi hapa Bungeni na nje ya Bunge hili. Nimeijua nchi yangu, nimejua siasa na nimejulikana ndani na nje ya Tanzania. Muhimu zaidi ni kwamba nimepata fursa adhimu ya kutoa mchango wangu katika kutunga sheria na sera mbalimbali kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu. Aidha, nilipata fursa ya kipekee kama Mbunge na Mwenyekiti wa Kamati zako mbili ya kuisimamia, kuishauri na kuiajibisha serikali.

4) Mheshimiwa Spika, Ninawashukuru sana wanachama wa CHADEMA kwa dhamana mbalimbali walizonipa ndani ya CHADEMA. Ninawashukuru viongozi wangu na hasa Mwenyekiti wetu Mheshimiwa Freeman Mbowe kwa kunilea na kuniamini kufanya naye kazi kwa kipindi chote tangu nilipokuwa mwanafunzi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, katika chama na hapa Bungeni. Kama ambavyo nimesema mara nyingi, CHADEMA imenilea na kunikuza tangu nikiwa na umri wa miaka 16 na tangu kipindi hicho nimejifunza mengi.

5) Mheshimiwa Spika, Nichukue nafasi hii kuwashukuru sana wananchi wa Kigoma Kaskazini kwa mapenzi yao na imani waliyonipa na kuniwezesha kukalia KITI hiki ninachokalia ndani ya Bunge lako Tukufu. Nashukuru kwamba juzi nilipata fursa ya kipekee ya kuwashukuru kwa imani waliyonipa kuwatumikia kwa vipindi viwili mfululizo. Mola atawalipa wananchi wa Kigoma Kaskazini kwa imani kubwa walioionyesha kwangu na kuniwezesha kulitumikia Taifa langu kwa namna nilivyolitumikia.

6) Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu sasa pamekuwa na msuguano wa kiuongozi kati yangu na viongozi wangu ndani ya CHADEMA uliosababishwa na tofauti za kimtazamo juu ya tafsiri pana ya demokrasia ndani ya chama chetu. Hatimaye tofauti hizi zilipelekea mwezi Novemba 2013 Kamati Kuu ya CHADEMA kunivua nafasi zangu zote za uongozi nilizokuwa nazo. Sikuridhika na maamuzi hayo na hivyo nikaonyesha kusudio la kukata rufaa katika Baraza Kuu la chama chetu kama taratibu za kikatiba za chama chetu zinavyotaka. Bahati mbaya ofisi ya Katibu Mkuu haikunipa fursa hiyo, na huo ndio ukawa msingi wa mimi kufungua kesi mahakamani kuweka pingamizi la Kikao cha Kamati Kuu kujadili hatima ya uanachama wangu hadi pale ofisi ya Katibu Mkuu itakaponipa fursa ya kukata rufaa katika vikao vya chama. Yaliyotokea baada ya hapo ni historia, lakini hatimaye Mahakama Kuu imetoa hukumu yake tarehe 10 Machi 2015. Katika hukumu hii, nimeshindwa kwa sababu za kiufundi kwa maelezo kwamba pingamizi letu liliwasilishwa kimakosa.

Pamoja na kwamba hatukuridhika na mwenendo wa jinsi kesi hii ilivyoamuliwa pamoja na maudhui ya hukumu yenyewe, ninaheshimu maamuzi ya mahakama na sina mpango wa kukata rufaa.

7) Mheshimiwa Spika, katika hali ya kawaida na kwa mujibu wa katiba ya chama chetu, ilitarajiwa kwamba baada ya maamuzi ya Mahakama Kuu, Kamati Kuu ingekaa na kunipa rasmi mashtaka yangu yanayohusu uanachama wangu, mimi kuitwa kujieleza na hatimaye Kamati Kuu kutoa uamuzi wake. Hata hivyo, mara baada ya hukumu ya Mahakama Kuu dunia nzima ilitangaziwa na Mwanasheria wetu Mkuu, kwa niaba ya chama, kwamba mimi nimeshafukuzwa na sio mwanachama tena wa CHADEMA. Baada ya hapo viongozi wangu wametoa matamko mbalimbali yote yakionyesha kwamba sitakiwi tena katika chama hiki, pamoja na kwamba hadi ninapoongea hapa leo sijawahi kukabidhiwa barua yeyote inayonitaarifu kufukuzwa kwangu katika chama.

8) Mheshimiwa Spika, kutokana na maelezo ya hapo juu, ni wazi kwamba uanachama wangu wa kisiasa ndani ya CHADEMA umeshaondolewa. Ninaweza kuendelea kupigania uanachama wangu kisheria na kwa kweli nina sababu na misingi yote kubaki na uanachama wangu kisheria. Lakini mimi ni mwanasiasa. Sikuja hapa bungeni kwa sababu ya kushinda kesi mahakamani. Nilichaguliwa na wananchi wa Kigoma Kaskazini na ninatambua kwamba huwezi kuwa mbunge bila udhamini wa chama cha siasa. Huu ndio utaratibu wa kisheria tuliojiwekea. Kwa mujibu wa viongozi wangu katika chama ni kwamba udhamini wa chama changu umekwishaondolewa.

9) Mheshimiwa Spika, kutokana na maelezo ya hapo juu, ninaomba kukutaarifu wewe na Bunge lako tukufu kwamba sina mpango wa kuendelea kupigania uanachama wangu wa CHADEMA katika viunga vya mahakama. Kwa hiyo ninatangaza rasmi leo kwamba taratibu za kikatiba zitakapokamilika tu nitaachia uanachama wa CHADEMA, chama nilichokipenda sana kwa sababu ya kuendelea kukua kwa tofauti za kiitikadi, kimtazamo na hata kibinafsi kati yangu na viongozi katika chama changu. Nimeona kuwa kuendelea kupigania uanachama kisheria ni kutatiza na kukwaza harakati za mabadiliko hapa nchini katika wakati ambapo mfumo wa kisiasa unatambua uwepo wa vyama vingi vya siasa. Kwa kuwa taratibu hizo sijui zitakamilika lini, natumia fursa hii kuwaaga wabunge wenzangu.

10) Mheshimiwa Spika, vyama vya siasa ni jukwaa muhimu katika ujenzi wa demokrasia lakini havipaswi kamwe kuwa juu ya wananchi. Kwa hiyo ni maoni yangu kwamba wakati sasa umefika wa kukomesha udola na ufalme wa vyama vya siasa hapa nchini. Mfumo wa siasa ambao unavipa vyama vya siasa mamlaka ya kisheria ya kukanyaga mamlaka ya wananchi haupaswi kuendelea katika Karne ya 21 na katika nchi ambayo inaendeshwa kwa misingi ya demokrasia ya kuheshimu wananchi. Mimi ninaondoka bungeni sio kwa sababu wananchi wangu wa Kigoma Kaskazini walionichagua wametaka niondoke. Siondoki kwa sababu nimeshindwa kufanya kazi zangu za ubunge. Na kwa kweli siondoki kwa sababu wanachama wenzangu katika CHADEMA wametaka niondoke. Ninaondoka kwa sababu mfumo wetu wa kisheria unavipa vyama vya siasa mamlaka juu ya wananchi na wapiga kura. Ni matumaini yangu kwamba Bunge lako tukufu halitaruhusu mfumo huu unaoruhusu vyama vya siasa kupora mamlaka ya wananchi uendelee. Ni Bunge lako pekee lenye uwezo wa kukomesha mfumo ambao unatukuza Parties’ Power, badala ya People’s Power.

11) Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema awali kwamba vyama vya siasa ni jukwaa. Bahati nzuri nchi yetu inafuata mfumo wa vyama vingi vya siasa na sasa tuna vyama 22. Kwa hivyo, wananchi wanaoniunga mkono wasisikitike kwa maamuzi yangu ya leo. Bado ninayo fursa ya kuwatumikia kupitia jukwaa lingine ambalo nitaamua katika siku chache zijazo, na inshala Mungu akitujalia nitarudi tena hapa Bungeni katika Bunge la 11 kwa nguvu za wananchi.

12) Mheshimiwa Spika, kwa miaka kumi niliyotumikia hapa Bungeni, si yote niliyoyafanya yalikuwa sahihi, yapo ambayo niliyakosea kama mwanadamu katika kufanya kazi zangu, kwa namna yeyote ile naomba radhi Watanzania wote kwa yote ambayo sikuyafanya kwa usahihi. Mimi ni binadamu, kiumbe dhaifu, sijakamilika. Ni Mola peke yake aliyekamilika.

13) Mheshimiwa Spika, siwezi kuanza maisha yangu mapya kisiasa bila ya kulishukuru Bunge lako Tukufu. Kwanza, Bunge la Tisa chini ya Mzee Samwel Sitta, mzee wa kasi na viwango! Bado ninakumbuka vizuri jinsi hoja ya Buzwagi ilivyotikisa Bunge lake na hatimaye kupelekea nchi yetu kufanya mabadiliko makubwa katika mfumo wa uendeshaji wa sekta ya madini (Sera mpya ya Madini na Sheria mpya ya Madini ) na hivyo kukuza mapato ya sekta ya madini kutoka Tshs. 32 bilioni kwa mwaka mpaka Tshs. 450 bilioni kwa mwaka.

14) Mheshimiwa Spika, ninajivunia kuwa sehemu ya Bunge la Kumi chini yako, Mama shupavu Anna Semamba Makinda. Katika Bunge hili nimekuzwa, nimejifunza, nimepambana, nimefurahi na nimelia ndani ya Bunge hili. Kwa pamoja tumepigania maslahi ya wananchi wetu kwa juhudi na maarifa na hivyo kuleta mabadiliko kadhaa. Ni katika kipindi hiki ambapo wabunge tumekuwa na sauti. Bunge la Tisa lilijijenga likawa ‘Bunge lenye Meno’ katika kupambana na ufisadi. Bunge la Kumi limejenga ‘Bunge lenye Nguvu’ katika mfumo wa Bajeti ya nchi yetu. Kupitia Bunge hili tumeweka misingi ya kujenga mfumo madhubuti wa uwajibikaji katika nchi yetu. Na katika siku za hivi karibuni Bunge la Kumi litakumbukwa kwa Hoja Maalumu ya Tegeta Escrow iliyopelekea mfumo wetu wa maadili ya Viongozi kupitia Baraza la Maadili kuanza kufanya kazi kwa namna ambayo haijawahi kushuhudiwa katika miaka iliyopita.

15) Mheshimiwa Spika, wajumbe wa PAC ( ambao nimeishi nao kama familia ) tumekuwa nguzo kubwa ya kujenga uwajibikaji wa Serikali kwa Bunge na wananchi. Napenda kuwashukuru kwa dhati kabisa kwa kuniunga mkono na kwa kunipa ushirikiano kama Mwenyekiti wao. Changamoto na malezi mliyonipa kwa miaka yote hii yamejenga Mtanzania mmoja mwenye nia ya dhati ya kuitumikia nchi yake, muda wowote, wakati wowote na kwa namna yeyote ile bila woga wala upendeleo. Nawashukuru kwa kujitoa kwenu kwa nchi yetu na dhamira isiyo na mawaa ya kujenga Taifa imara zaidi. Pamoja na kwamba ninaondoka Bungeni leo, ninaahidi kuendelea kuwatumikia wananchi wa Kigoma Kaskazini na Taifa langu katika kusimamia ukweli, kutetea demokrasia ya kweli na kupigania maendeleo ya kweli kwa mwananchi wa kawaida bila ubaguzi wowote.

16) Mheshimiwa Spika, Kwa viongozi na wanachama wa CHADEMA, najivunia kwa fursa mliyonipa kuwa sehemu ya Baraza hili la Taifa ambalo leo ninalihutubia kwa mara ya mwisho kama mbunge wa Kigoma Kaskazini. Inawezekana tusiweze kuelewana katika masuala ya uongozi, misingi na itikadi, lakini ninaamini tunapaswa kuelewana na kukubaliana katika dhamira kubwa ya kuijenga nchi yetu kuwa Taifa linalojitegemea na lisilo na aina yeyote ya ubaguzi. Taifa lenye uchumi shirikishi wenye kuzalisha ajira na kuondoa umasikini, ujinga na maradhi, yaani Taifa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Na ni matumaini yangu kuwa tutakuwa bega kwa bega katika harakati hizi katika siku zijazo. Yaliyopita si ndwele tugange yajayo. Nafasi hii ya kihistoria tuliyopewa haihitaji siasa za ubinafsi na unafsi! Uzalendo wetu utapimwa kwa uwezo wetu wa kuweka tofauti zetu binafsi pembeni kwa lengo lililo kubwa zaidi yetu.

17) Mheshimiwa Spika, Ninawashukuru tena na tena wana Kigoma na wananchi wote wa Tanzania ambao kwa ridhaa yao nimekaa katika viti hivi kwa miaka takribani kumi. Ninawahakikishia kuwa changamoto nilizokumbana nazo na ambazo zimenilazimisha leo niondoke bungeni zimechochea zaidi dhamira, nia na sababu yangu ya kuwatumikia kwa nguvu zaidi kuliko wakati mwingine wowote ule. Huu ni mwanzo mpya.

Mheshimiwa Spika,

Asanteni sana na Kwa herini!