Monday , 3rd Sep , 2018

Taasisi ya wanaharakati wa kutetea haki za wanyamapori nchini Botswana, wamegundua mabaki ya mizoga ya tembo taribani 90 karibu na hifadhi moja maarufu nchini humo.

Mabaki ya mizoga ya tembo.

Taasisi hiyo ya Elephants Without Borders, ambayo inafanya utafiti kuhusu wanyamapori, imesema kiwango cha vifo hivyo kutokana na ujangili ni kikubwa kuwahi kushuhudiwa barani Afrika.

Wanasayansi wanaofanya utafiti huo wamesema tembo 87 waliuwawa wiki chache zilizopita kwa ajili ya meno yao, ambapo pia faru weupe watano waliuwawa miezi mitatu iliyopita.

"Nimeshstushwa na kushangazwa na kiwango hiki cha ujangili ambacho sijawahi kukishuhudia Afrika", amesema, Dkt. Mike Chase wa Elephants Without Borders.

Kwa mujibu wa sensa kubwa ya tembo iliyofanyika mwaka 2015, inakadiriwa kwamba, theluthi ya tembo barani Afrika wameuwawa katika kipindi cha muongo mmoja uliopita huku asilimia 60 ya tembo nchini Tanzania wakitoweka katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.