Monday , 4th Aug , 2014

Tume ya Kudhibiti UKIMWI nchini Tanzania (TACAIDS), imesema inaandaa mwongozo wa utoaji wa huduma za kuzuia maambukizi mapya kwa makundi na watu walio katika hatari zaidi ya kupata maambukizi ya virusi HIV vinavyosababisha Ukimwi.

Waziri wa nchi ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge.

Mwenyekiti wa Tume hiyo, Dkt Fatma Mrisho amesema hayo leo jijini Dar es Salaam ambapo ameyataja makundi hayo kuwa ni ya watu wanaojihusisha na biashara ya ngono, wanaofanya mapenzi ya jinsia moja, watumiaji wa dawa za kulevya pamoja na madereva wa safari ndefu ambao wengi wao wamekuwa na mpenzi zaidi ya mmoja.

Dkt. Mrisho ametaja moja ya huduma hizo kuwa ni pamoja na elimu maalum juu ya hatari inayoyakabili makundi hayo, matumizi ya njia sahihi za kujilinda dhidi ya maambukizi mapya pamoja na mafunzo ya kuacha vitendo na tabia hatarishi ikiwemo matumizi ya dawa za kulevya na ulevi wa kupindukia.

Wakati huo huo, Tanzania imetajwa kuwa ni moja ya nchi ambayo imefanikiwa katika mapambano dhidi ya ugonjwa hatari wa UKIMWI hivyo hakuna budi kutoa kipaumbele zaidi kwa makundi hasa ya vijana ambayo yameonekana kutozingatia matumizi sahihi ya kinga dhidi ya ugonjwa huo.

Waziri wa nchi, Ofisi wa Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge Mh. William Lukuvi amesema hayo jijini Dar es Salaam wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu nini kimejiri wakati ujumbe wa Tanzania uliopohudhuria mkutano wa 20 wa Kimataifa kuhusu UKIMWI uliofanyika nchini Australia.