
Mbunge wa Ukonga Mwita Waitara
Miongoni mwa wabunge ambao wameapishwa jumatatu ya wiki hii wabunge watatu kati yao walikuwa wanatokea vyama vya Upinzani likiwemo Jimbo la Ukonga, Mwita Waitara ambaye alikuwa moja ya wabunge wenye msimamo mkali kutoka Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
www.eatv.tv imefuatilia mienendo ya mbunge huyo kabla ajahamia chama chake kipya na namna alivyokuwa akiishurutisha serikali katika kipindi cha miaka 2 na nusu ambayo amelitumikia Bunge hilo kama mpinzani na miaka 2 na nusu atakayolitumikia akiwa Chama Tawala.
Kwa mara ya kwanza Waitara alishinda kwenye uchaguzi Mkuu 2015 kupitia CHADEMA ambapo kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) vipaumbele vya kiongozi huyo vilikuwa ni kupigania kwa kile walichokiamini kuwa ni demokrasia, katiba mpya, pamoja na tume huru ya uchaguzi.
July 28 mwaka huu Mbunge huyo alijitokeza kwenye mkutano wa Katibu wa Itikadi na Uenezi Humphrey Polepole wakati akizungumza na waandishi wa habari na kutangaza kujivua nafasi yake ya kujiunga na CCM kwa madai ya kuwa na mgogoro na Freeman Mbowe.
Novemba 05 mwaka huu Mbunge huyo aliapishwa kama mbunge mpya wa Chama Cha Mapinduzi na kupelekea kuwa na sura nyingine ikiwemo ya kupinga kuwepo kwa katiba mpya na kushinikiza utekelezwaji wa miradi ya maendeleo.
"Haya yanayofanyika hayahitaji katiba mpya, wale wanaosubiri katiba mpya waendelee kusubiri tu katiba ila haya yatekelezwe watu wanataka huduma za kijamii na sio katiba mpya, hayo maneno ya katiba mpya ni ya upinzani sio wananchi," alisema Waitara.
Mfululizo wa matukio na kauli za mbalimbali za kiongozi huyo kunaonesha kuwa ameonesha dhahiri sura zake mbili katika kipindi cha muda wote huo, huku ikionekana wazi kuwa msimamo wake hivi sasa uko tofauti na msimamo wake wa awali.