Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Hifadhi ya Jamii nchini Tanzania (SSRA) Bi. Irene Kisaka (kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Idara ya Habari, Mawasiliano na Elimu kwa Umma wa Mamlaka hiyo Bi. Sarah Kibonde.
Viongozi hao ni wale wa kutoka Chama cha Walimu CWT, Chama cha Wafanyakazi wa Afya na Serikali Kuu (TUGHE) pamoja na chama cha wafanyakazi wa serikali za mitaa (TALGWU), vyama ambavyo katika siku za hivi karibuni vimekuwa vikilalamikia mfumo huo mpya kuwa umelenga kupunguza mafao ya pensheni.
Katika maelezo yake ya ufunguzi wa mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu wa SSRA Bi. Irene Kisaka amesema lengo la mkutano huo ni kuelimisha wadau juu ya mfumo huo, ili nao wakawaelimishe wanachama wao waachane na uvumi unaoenezwa kuwa mfumo mpya wa kukokotoa mafao utapunguza kiwango cha pensheni ambacho mstaafu anastahili kupata.
Kwa mujibu wa Bi. Kisaka, baada ya mkutano wa leo, SSRA kwa kushirikiana na viongozi wa vyama hivyo katika ngazi ya mikoa, watazunguka nchi nzima kutoa elimu kwa watumishi kuhusu mfumo huo mpya uliopitishwa na serikali Juni mwaka huu.
Tofauti na ambavyo imekuwa ikizungumzwa, Bi. Kisaka amesema mfumo huo mpya umelenga kuboresha mafao ya wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii na sio kupunguza mafao yao kama ambavyo baadhi ya watu wamekuwa wakipotosha.
Hata hivyo, baada ya kupitia sehemu ya vipengele muhimu vya mfumo huo, EATV imebaini kuwa mabadiliko ya mfumo wa kikokotozi, itahusisha wanachama waliojiunga na huduma za hifadhi ya Jamii baada ya mwezi Juni mwaka huu na kwamba wanachama wote, wakiwemo watumishi wa umma na wa sekta binafsi ambao walikuwa wanachama wa moja ya mifuko ya hifadhi kabla ya Juni mwaka huu hawataathiriwa na mabadiliko hayo mapya.
Mkutano wa leo umehudhuriwa pia na mwakilishi wizara ya kazi na ajira ambaye sehemu ya maazimio ya mkutano wa leo yatawasilishwa serikalini kwa ajili ya hatua zaidi.