Thursday , 17th Dec , 2015

Waziri Mkuu wa Japan Mhe. Shinzo Abe amemtumia salamu za pongezi Rais wa Tanzania kwa kuchaguliwa kwake kuwa Rais wa awamu ya tano na kumuahidi kuwa Japan itaendelea kushirikiana na Tanzania katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na maendeleo.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kulia akiagana na Balozi wa Japan Nchini Mheshimiwa Masaharu Yoshida

Akiwasilisha ujumbe maalum wa maandishi kutoka kwa Mheshimiwa Abe, Mjumbe Maalum kutoka Japan ambaye ni waziri wa nchi anayeshughulikia mambo ya nje ya Japan Bwana Seiji Kiara amemueleza Rais Magufuli kuwa Japan imeridhishwa na hatua ambazo serikali ya Tanzania inazichukua katika kuharakisha utekelezaji wa miradi hiyo na ameahidi kuongeza msukumo kwa upande wa Japan katika kuharakisha utekelezaji wa miradi inayofadhiliwa na Japan.

Juzi (15 Novemba, 2015) Mjumbe huyo Maalum kutoka Japani ameshuhudia utiaji saini wa makubaliano ya ujenzi wa njia ya umeme yenye urefu wa kilometa 441.5 kutoka Singida - Manyara - Namanga na kuunganisha hadi Kenya ambapo Japan imetoa mkopo wa dola milioni 96 ili kufanikisha mradi huo

Akizungumza baada ya kuagana na mjumbe huyo maalum kutoka Japan, Rais Magufuli amesema, kwa kuwa Tanzania inaelekea kuwa na umeme wa ziada, mradi huo ukikamilika utaiwezesha kuuza umeme nje nchi.

Kuhusu ujenzi wa mtambo wa kuzalisha umeme wa gesi wa Kinyerezi namba mbili ambao Japan imetoa mkopo wa dola za Marekani milioni 292 kwa ajili ya kuutekeleza, Rais Magufuli amesema baada ya kubana matumizi katika bajeti ya serikali, wiki hii Tanzania itakamilisha utoaji wa kiasi cha dola za kimarekani milioni 51.8 ambazo ni sawa na asilimia 15 ya fedha zote zitakazogharamia ujenzi huo.

Aidha Rais Magufuli amesema taratibu za kuanza ujenzi wa barabara ya juu yaani "Flyover" katika makutano ya barabara ya Tazara zimeanza na kwamba jiwe la msingi linatarajiwa kuwekwa mwezi Januari, na kwamba fedha kwa ajili ya ujenzi Flyover hiyo ya kwanza hapa nchini zipo na mkandarasi ameshalipwa fedha za awali.

Dkt. Magufuli pia amezungumzia ujenzi wa barabara nyingine mbili ambazo ni ya Gerezani - Bendera tatu itakayokuwa na Flyover katika eneo la Kamata na Barabara ya Mwenge - Morocco na kwamba Japan imeahidi kutangaza tenda hizo hivi karibuni.

Amesema tayari Tanzania imeanza ujenzi wa njia mbili za barabara ya Mwenge - Morocco katika upande wa kulia yenye urefu wa kilometa 4.3 kwa kutumia fedha zake zilizopatikana baada ya kuahirisha shamrashamra za sikukuu ya Uhuru na kwamba Japan itajenga njia zingine tatu upande wa kushoto na hivyo kuifanya barabara hiyo kuwa na njia tisa.

Katika Hatua nyingine Rais Magufuli amempongeza Kaimu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania Dkt. Philip Mpango kwa kazi nzuri ya ukusanyaji wa mapato inayofanywa na mamlaka hiyo ambayo imeongeza ukusanyaji wa Mapato na kwa mara ya kwanza mwezi huu ukusanyaji wa mapato hayo unatarajiwa kuwa zaidi ya shilingi Trilioni 1 na Bilioni 300.

Kutokana na mafanikio hayo amewahakikishia watanzania kuwa fedha kwa ajili ya kutimiza ahadi ya kutoa elimu bure kwa shule za msingi na sekondari ambazo ni kiasi cha shilingi Bilioni 131 zitatengwa mwezi huu na kupelekwa moja kwa moja katika shule husika.

Amesema wakurugenzi wa Halmashauri, Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa watapatiwa nakala za taarifa za ugawaji wa fedha hizo na kuonya kuwa hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote atakayethubutu kuzitumia vibaya.

Dkt. Magufuli ameongeza kuwa fedha hizo ambazo ni pamoja na fedha za maendeleo, fedha za mitihani na fedha vifaa vya kufundishia zitaanza kutumwa kila mwezi kuanzia mwezi huu wa kumi na mbili