Mganga Mkuu wa serikali ambaye ni Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Dkt Donnan Mmbando.
Kaimu Katibu Mkuu ambaye pia ni Mganga Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Dkt Donnan Mbando, amesema hayo leo katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, hasa kuhusiana na taarifa zilizozagaa wiki iliyopita kwamba mtu mmoja ameripotiwa katika zahanati ya Shirimatunda mkoani Kilimanjaro, akiwa na dalili za ugonjwa huo.
Kwa mujibu wa Dkt Mmbando, mgonjwa huyo ambaye hadi hivi sasa amelazwa katika zahanati ya Shirimatunda, hana ugonjwa wa Ebola kama ambavyo imekuwa ikidhaniwa, bali yupo hospitalini hapo akitibiwa ugonjwa wa malaria.
Aidha, Dkt Mmbando amewataka wananchi kutokuwa na hofu, badala yake waendelee kuchukua tahadhari za kuepuka kupata maambukizi ya ugonjwa huo, tahadhari inayohusisha kuepuka kugusa au kuingiwa na mate, damu, mkojo, jasho, kinyesi, machozi na majimaji mengine yanayotoka mwilini mwa mtu mwenye dalili za ugonjwa wa Ebola.
Tahadhari nyingine ni kuepuka kushughulikia maiti ya mtu aliyekufa akiwa na dalili za ugonjwa wa ebola na kwamba endapo kitatokea kifo kinachotiliwa shaka, basi watoe taarifa kwa uongozi wa kituo cha huduma za afya kwa ushauri ambapo wataalam watasimamia maziko ya mtu huyo iwapo kitatokea.