Wednesday , 21st Oct , 2015

Licha ya sekta ya madini kuchangia asilimia 3.5 kwenye pato la Taifa wakazi wa Arusha wamesema kuwa mchango huo bado hauridhishi ukilinganisha na uzalishaji wa madini katika sekta hiyo nyeti hivyo wameitaka serikali iongeze usimamizi.

Waziri wa nishati na madini Mh George Simbachawene

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi hao wamesema kuwa bado kuna changamoto ya kukosekana kwa uwazi katika sekta ya madini kwani watanzania wengi hawajui ukweli juu ya rasilimali hizo na namna ambavyo zinachangia maendeleo ya taifa.

Mkazi wa Arusha Ibrahim Henry amesema kuwa bado watanzania wana uelewa mdogo juu ya sekta ya madini na uendeshaji jambo linalowafanya kutokuona fursa zilizopo katika sekta hiyo na kunufaika nazo.

Lucas Myovela amesema kuwa bado mchango wa sekta ya madini ni mdogo na hauridhishi kwa taifa suala linalochangiwa na usimamizi mbovu wa rasilimali za madini ambazo zingeweza kusaidia kupunguza umasikini nchini na kuinua sekta nyingine ikiwemo kilimo na elimu.

Mkazi wa Arusha Arnold Rweyemamu amesema kuwa ili sekta ya madini iweze kulinufaisha taifa serikali haina budi kuziba mianya ya utoroshwaji wa madini ambayo hayapiti kwenye mfumo rasmi hivyo kupoteza mapato ambayo yangesaidia kukuza uchumi wa nchi.

Mbali na juhudi zinazofanywa na serikali kuhakikisha kuwa sekta hiyo inaendeshwa kwa uwazi bado juhudi zaidi zinahitajika na kuweka sera ambazo zitasaidia kudhibiti rasimali hizi zitumike kubadilisha uchumi wa nchi kwa kiwango stahiki.