Monday , 18th Apr , 2016

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ameongoza sherehe za kuwasha Mwenge wa Uhuru mkoani Morogoro huku akisema serikali imeweka mikakati thabiti kuwasaidia vijana katika ushiriki wa kukuza uchumi wa nchi.

Makamu wa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Samia Hassan Suluhu,

Akizungumza leo mkoani Morogoro Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa serikali itaweka mazingira wezeshi kwa vijana kwa kushiriki na kushirikishwa katika ngazi mbalimbali za maamuzi ili kuleta maendeleo ya nchi.

Mhe. Samia amewataka vijana kuchangamkia fursa zitolewazo na serikali katika juhudi za kujiletea maendeleo ikiwa ni pamoja na fusra za kibiashara, kiuongozi na mengineyo.

Aidha Makamu huyo wa Rais amesema kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012 vijana kati ya miaka 15 hadi 35 ni milioni 16. 2 ambayo ni sawa na asilimia 31 ya watu wote nchini huku nguvu kazi yao ikitegemewa kwa asilimia 59, hivyo serikali haina budi kuwashirikisha katika kukuza uchumi wa nchi.

Mhe. Samia amesema kuwa tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana linasababishwa na mambo kadhaa ikiwemo kasi ndogo ya ukuaji wa nafasi za ajira katika uchumi na ukosefu wa miundombinu muhimu ya kiuchumi kama vile viwanda, nishati na uchukuzi.

Aidha Bi. Samia amesema tatizo la ajira nchini kwa mujibu wa takwimu za ajira nchini zinaonesha kiwango cha ukosefu wa ajira kwa watu wenye uwezo wa kufanya kazi asilimia 10.3 ingawa takwimu hizi zinaonesha ukosefu wa ajira kwa vijana umepungua lakini bado jitihada zinahitajika kupunguza zaidi tatizo hilo.

Takwimu pia zinaonesha kuwa tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana lipo zaidi mijini ambapo ni asilimia 18.3 ikilinganishwa na asilimia 8.6 kwa vijana waishio vijijini huku takwimu hiyo ikiwa inawaathiri vijana wa kike.

Mhe. Samia amesema katika kukabiliana na changamoto hiyo wameanza na kurekebisha mfumo wa elimu na kuendeleza ujuzi ili kuwezesha nguvu kazi inayoingia katika soko la ajira kuwa na uwezo wa kumudu mazingira ya sasa ya ushindani.

Katika uzinduzi huo, viongozi mbalimbali wa serikali, dini na vyama vya siasa wamealikwa kushiriki wakiwemo pia mawaziri wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano ambapo kauli mbiu ya mwaka huu inasema "Vijana ni nguvu kazi ya taifa washirikishwe na wawezeshwe"

Sauti ya Makamu wa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Samia Hassan Suluhu wakati wa uwashaji wa Mwenge wa Uhuru