Friday , 25th Sep , 2015

Serikali mkoani Morogoro imeahidi kuendelea kuunga mkono jitihada mbalimbali zinazofanywa na wadau wa maendeleo,wakiwemo wanaosaidia kufikisha nishati mbadala ya umeme kwa gharama nafuu kwenye maeñeo yanayotoa huduma muhimu za kijamii.

Mkuu wa mkoa wa Morogoro Dkt.Rajab Rutengwe

Mkuu wa mkoa wa Morogoro Dkt. Rajab Rutengwe amesema hayo baada ya kuzindua ujio wa kampuni ya M-Power Tanzania,inayohusika na usambazaji wa umeme nje ya gridi ya taifa, ambapo mbali na kuwahimiza viongozi wa ngazi mbalimbali kutoa ushirikiano kuhakikisha tatizo la nishati ya umeme linaondoka katika maeneo yao na kupongeza kampuni hiyo kuzalisha ajira zaidi ya 500.

Dkt. Rutengwe ameita kampuni hiyo kuuza umeme kwa gharama nafuu ili mwananchi wa kawaida aweze kumudu,na kupanua wigo wa mahitaji ya umeme huo ili kuwafanya wananchi hasa wa maeneo ya vijijini waweze kujiajiri.

Kwa upande wake kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro Leonard Paul akiomba kampuni hiyo kutoa huduma hiyo kwa vituo vidogo vya polisi ambavyo havina umeme.

Mkurugenzi wa usambazaji M-Power Tanzania, Raphael Robert, amesema kampuni hiyo iliyoanza kazi zake kwa nchi za Tanzania na Rwanda ikilenga kutoa umeme mbadala kwa minara ya makampuni ya simu, ilibaini ipo haja ya kuwasaidia watanzania wengi zaidi hasa baada ya kubaini changamoto ya matumizi ya mafuta ya taa na mishumaa hasa kwa wanafunzi wanaoishi maeneo yasiyofikiwa na umeme wa gridi ya taifa.

Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa mpaka sasa wameshafikia mikoa 13 nchini nia ikiwa na lengo la kuiangaza Tanzania nzima na hata bara zima la Afrika.

Tayari wananchi wa kata za Kihonda na Kihonda Maghorofani wanaoishi mitaa ambayo haijafikiwa na umeme wa gridi ya taifa ikiwemo mitaa ya Yespa, Magereza na nguvu kazi wameanza kufaidika na umeme huo mbadala.